RAIS John Magufuli amesema aliamua kupeleka Muswada wa Marekebisho ya Sheria Mbalimbali wa Mwaka 2017 kuhusu ya madini bungeni, kwa hati ya dharura ili kutetea rasilimali za nchi ili ziwanufaishe Watanzania wote.
Dk Magufuli aliyasema hayo jana mjini hapa mkoani Mwanza, wakati akizindua rasmi mradi mkubwa wa maji wa Nyamazugo uliojengwa kwa gharama ya Sh bilioni 21 ambao unatarajia kuwanufaisha jumla ya watu 138,000, ambapo aliwataka wakazi wa Sengerema kuilinda na kuutunza mradi huo.

Aliwashukuru Washirika wa Maendeleo, Benki ya Maendeleo ya Afrika, Kamisheni ya Bonde la Ziwa kwa nchi za Afrika Mashariki na Wizara ya Maji na Umwagiliaji kwa kazi kubwa waliyofanya kwa kukamilisha ujenzi wa mradi huo.
Kuhusu kauli yake ya wanafunzi wanaopata ujauzito shuleni, alisema uamuzi wake uko palepale na kuonya kuwa mkuu wa shule yoyote atakayeruhusu msichana aliyepata ujauzito atasimamishwa kazi.
“Tukiijenga principle (kanuni) hii, ya watoto kujifungua na kurudishwa shuleni, hakuna mtoto wa kike atakayesoma,” alieleza. Alisema serikali yake haiwezi kuwasomesha wasichana kwa fedha za walipa kodi na badala yake akayataka mashirika yasiyo ya kiserikali na wanaharakati wanaopigia debe suala la wanafunzi wajawazito kurudi shule, wafungue shule zao ili wawasomeshe wanafunzi wanaopata ujauzito.
Kuhusu safari za nje, alisema hadi sasa amekataa mialiko ya safari za nje ya nchi ipatayo 60, kwani ameona ni vyema kwanza ashughulikie changamoto za ndani ya nchi. “Hata jana (juzi) ilitakiwa niende Ethiopia, lakini nimetuma Makamu wa Rais ameenda huko,” alifafanua na kuongeza kuwa yeye ni Yohana Mbatizaji anayefanya kazi ya kumsafishia njia Rais ajaye kwa kuondoa uovu katika maeneo mbalimbali nchini.
Kwa upande wake, Katibu Mkuu Wizara ya Maji na Umwagiliaji, Profesa Kitila Mkumbo alisema mradi huo uliozinduliwa na Rais Magufuli ni sehemu ya programu ya uboreshaji wa huduma za maji kwa miji 15 ya nchi za Afrika Mashariki, ambapo kwa Tanzania programu hiyo imetekelezwa kwa miji ya Sengerema, Geita, Nansio na Sirari.
Profesa Mkumbo alisema mradi huo umekamilika na utawawezesha wananchi kupata huduma ya maji safi na kunywa kwa asilimia 100, ambapo awali huduma hiyo kwa asilimia 33. Naye Waziri wa Maji na Umwagiliaji, Gerson Lwenge alisema serikali imeikabidhi Mamlaka ya Maji Safi na Usafi wa Mazingira kuusimamia mradi huo. Alisema serikali pia iko katika hatua ya mwisho ya utekelezaji wa miradi mingine ya maji nchini ukiwemo mradi wa Mji wa Geita unaotarajiwa kugharimu zaidi ya Sh bilioni sita.