BUNGE limepitisha sheria mpya ambayo sasa itatambua haki na dhamana ya serikali katika makinikia ambayo itakuwa ni marufuku kuchenjuliwa nje ya nchi na serikali itashiriki kwa asilimia kuanzia 16 hadi 50 katika shughuli zote za uchimbaji, uchakataji na uchejuaji madini na ununuzi wa hisa katika kampuni ya uchimbaji madini.

Aidha, Wakala wa Ukaguzi wa Madini (TMAA) umefutwa rasmi na sasa kunaanzishwa Kamisheni ya Madini, na kwamba kuanzia sasa umiliki wa leseni mbalimbali zinazotolewa kwa mujibu wa Sheria ya Madini, hautahamishwa kabla haujafanyiwa uendelezaji katika kitalu husika. Akielezea mapendekezo ya Muswada wa Sheria ya Marekebisho ya Sheria Mbalimbali wa Mwaka 2017 katika Sheria ya Madini ya Mwaka 2010, Waziri wa Katiba na Sheria, Profesa Palamagamba Kabudi alisema asilimia hizo za hisa ni kwa kuangalia thamani ya gharama ambazo serikali inahamia katika vituo vya uwekezaji na kodi aliyopewa mwekezaji. Profesa Kabudi alisema muswada huo pia unatambua haki na dhamana ya serikali juu ya makinikia na kuweka utaratibu wa kuyahifadhi sehemu maalumu migodini chini ya uangalizi wa serikali.
Makinikia marufuku nje “Kupitia marekebisho hayo, makinikia yanayotolewa nchini bila kufanyiwa uchunguzi wa kupata thamani halisi kabla ya kuchenjuliwa na uchenjuaji utafanyika nchini. Kuanzia sasa makinikia hayatauzwa nje ya nchi, yatauzwa kwenda kwa wachenjuaji wa ndani ya nchi yakiwa ni bidhaa ambayo itatozwa kodi,” alifafanua. Alisema pia muswada unaipa serikali haki na dhamana juu ya usimamizi wa bidhaa zote na maliasili, zinazotokana na uchimbaji, uchakataji na uchejuaji wa madini yakiwamo makinikia au kwa jina maarufu mchanga wa dhahabu.
Aidha, alisema muswada umelenga kutambua na kuweka chini ya uangalizi wa serikali maeneo yote ya uchimbaji na madini kwa lengo la kuweka ulinzi na usimamizi madhubuti wa madini kwa lengo la kuweka ulinzi na usimamizi madhubuti wa maeneo ya uchimbaji. “Hii itasaidia kuwepo ulinzimahsusi wa maeneo yote ya uchimbaji wa madini, kuwepo kwa utaratibu wa serikali kufanya ukaguzi na udhibiti wa usambazaji wa madini, kuipa serikali uwezo wa kudhibiti na kutambua viwango vya madini yote yanayotolewa kwenye maeneo ya migodi na kupitia vyombo vya ulinzi na usalama vya serikali,” alieleza.
TMAA yazikwa rasmi Alieleza kuwa kufutwa kwa TMAA kunatokana na majukumu yake, yaliyokuwa yakitekelezwa na wakala huyo kuhamishiwa kwa Kamisheni ya Madini ambayo itaanzishwa. Akiwasilisha muswada huo, Profesa Kabudi alisema kutokana na kufanyiwa mapitio ya madaraka ya Waziri na Kamishna wa Madini kwa lengo la kuwapunguza baadhi ya majukumu na madaraka yatahamishiwa kwa Kamisheni ya Madini.
Alisema kamisheni inayopendekezwa kuanzishwa itakuwa na jumla ya makamishina tisa, na watu kati yao akiwamo Mwenyekiti watakuwa wa kudumu. “Watashirikiana na watendaji wakuu kutekeleza majukumu yao ya Kamisheni ya kila siku, makamishna wengine watakuwa wa muda na watakutana katika vikao maalumu vya kamisheni kwa ajili ya kufanya maamuzi ya misingi na kufuatilia utekelezaji wake,” alifafanua na kuongeza kuwa makamishina wa muda watateuliwa kutokana na nafasi zao ambao ni Katibu Mkuu Hazina, Katibu Mkuu Tamisemi, Naibu Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Katibu Mkuu wa Ulinzi na Katibu Mkuu Ardhi.
“Kamisheni inayopendekezwa kuundwa itachukua majukumu sehemu kubwa ya majukumu ya Kamishna wa Madini kwa sasa. Majukumu hayo ni pamoja na kutoa, kuhuisha au pale itakapolazimika kufuta leseni zote zinazotolewa kwa mujibu wa sheria ya madini, kusimamia shughuli za madini ikiwa ni pamoja na kufanya ukaguzi maeneo ya migodi.
Pia majukumu yote yaliyokuwa yakitekelezwa na TMAA yatahamishiwa na kuwekwa chini ya Kamishna. Na kwa msingi huu TMAA inafutwa,” alibainisha. Umiliki wa leseni Kuhusu kutohamisha leseni, alisema hatua hiyo ni katika kuzuia watu kufanya biashara ya udalali wa leseni. “Katika kuweka masharti yanayokusudia kuzuia watu kufanya biashara ya udalali wa leseni mbalimbali zinazotolewa kwa mujibu wa sheria ya madini, mmiliki wa leseni hataruhusiwa kuhamisha umiliki wa leseni kabla ya uendelezaji katka kitalu husika,” alieleza. Aliongeza, “baada ya kumalizika kwa muda wake, leseni itahuishwa kwa kipindi kimoja tu, na baada ya hapo umiliki wa kitalu husika utarejeshwa serikalini.”
Aidha, muswada wa sheria umeainisha vyombo vitakavyohusika katika shughuli za madini ambavyo ni hifadhi ya dhabaru na vito chini ya Benki Kuu, kuanzishwa maeneo maalumu ya masoko ya dhahabu na vito, maghala ya serikali ya kuhifadhia madini, Kanzidata ya Taifa ya Raslimali za Madini na kuanzisha mfumo mahsusi wa kukusanya na kuhifadhi taarifa zote za shughuli za madini. Aidha, Kabudi alisema pia muswada umependekeza marekebisho ya Sheria ya Kodi ya Mapato kama sehemu ya mapato ya biashara faida yoyote inayopatikana kutokana na uhamishaji wa jukumu la kulipa kodi kupitia mikataba mbalimbali.
“Lengo ni kuondoa mianya ya upotevu wa mapato kutokana na kutowianisha Sheria ya Kodi ya Mapato na mifumo iliyopo chini ya mikataba ya mafuta na gesi,” alieleza. Akizungumzia Sheria ya Bima, alisema marekebisho yamekusudia kuondoa utaratibu wa sasa ambao kilawakala wa bima hujipangia kiwango cha ada anachotaka. “Ili kuondoa kasoro zilizopo sasa katika mfumo wa ukusanyaji wa ada ya bima kupitia mawakala wa bima.
Kwa mujibu wa mapendekezo, bidhaa zote zinazoingizwa nchini zitakatiwa bima na kampuni za bima za Tanzania,” alieleza. Maoni ya Kamati Mwenyekiti wa Kamati, Mohamed Mchengerwa alisema ni vema serikali ikashiriki katika hatua zote ambazo ni utafutaji, uchimbaji, uchenjuaji na uuzaji wa madini. “Hatua hii itaifanya serikali kusimamia kikamilifu shughuli za utafutaji wa madini ili kupunguza mianya ya udanganyifu katika taarifa za utafiti,” alieleza huku akishauri kufanyiwa marekebisho muudo wa tume kwa kuongeza uwakilishi wa wachimbaji wadogo, na wigo wa ushiriki wa Watanzania katika shughuli za madini na mafuta kama vile uuzaji wa bidhaa na huduma migodini, ajira kwa Watanzania katika migodi na nafasi za mafuta kwa vitendo kwa wanafunzi wa kitanzania.
Wabunge wachangia Mbunge wa Vunjo, James Mbatia (NCCR Mageuzi) alisema ni vyema kuweka maslahi ya Taifa mbele kwa kuwa kitu kimoja; wakati Mbunge wa Busanda, Lolensia Bukwimba (CCM) alishauri serikali asilimia 16 za hisa zilizoongezwa, asilimia moja ipelekwe kwenda kuimarisha maeneo ambayo madini yanayotokea. Mbunge wa Nzega Mjini, Hussein Bashe (CCM) alisema ni vema kwenye Kamisheni ya Madini, kukawa na uwakilishi wa wachimbaji wadogo, ambao ndio watakaosaidia kukuza biashara ya madini na kuepusha utoroshaji wa madini.
Mbunge wa Kiembesamaki, Ibrahim Raza (CCM) alisema Watanzania miaka yote walikuwa wanaibiwa kama vile walikuwa chumba cha wagonjwa wenye kuhitaji uangaliz maalumu (ICU) na kwamba Rais John Magufuli amewakomboa. Alipongeza serikali kwa udhibiti wa madini hadi maeneo ya migodi ili kutoibwa tena. Mbunge wa Temeke, Abdalla Mtolea (CUF), alisema inawezekana kuna wakati tatizo sio sheria, bali ni namna ambavyo serikali inazisimamia sheria hizo.