Naibu Waziri wa Kilimo Mifugo na Uvuvi Mhe William Tate Ole Nasha (Mb) akizungumza kwa niaba ya Waziri wa Kilimo Mifugo na Uvuvi Mhe Dkt Charles Tizeba wakati wa uzinduzi wa maadhimisho
ya sikukuu ya wakulima - Nanenane, mwaka 2017 katika viwanja vya
maonesho ya kilimo ya Ngongo Mkoa wa lindi, jana tarehe 1/8/2017. (Picha zote na Mathias Canal)



Naibu Waziri wa Kilimo Mifugo na Uvuvi Mhe William Tate Ole Nasha (Mb) alipotembelea banda la JKT kujionea namna ya uzalishaji mali unaofanywa na Jeshi hilo wakati wa uzinduzi wa maadhimisho
ya sikukuu ya wakulima - Nanenane, mwaka 2017 katika viwanja vya
maonesho ya kilimo wa Ngongo Mkoa wa lindi, jana tarehe 1/8/2017.


Naibu Waziri wa Kilimo Mifugo na Uvuvi Mhe William Tate Ole Nasha (Mb) (kulia) akizungumza jambo na Katibu
Mkuu wa Wizara ya Kilimo Mifugo na Uvuvi Mhandisi Methew J. Mtigumwe
wakati wa uzinduzi wa maadhimisho
ya sikukuu ya wakulima - Nanenane, mwaka 2017 katika viwanja vya
maonesho ya kilimo wa Ngongo Mkoa wa lindi, jana tarehe 1/8/2017.







Na
Mathias Canal, Lindi









Naibu
Waziri wa Kilimo Mifugo na Uvuvi, Mhe. Wiliam Tate Ole Nasha (Mb) amesema kuwa
kwa muda mrefu serikali imekuwa ikipata malalamiko kutoka kwa wananchi
mbalimbali hususani kwa wakulima nchini Tanzania wakipinga kodi na tozo
mbalimbali zinazotozwa kwani zimekuwa zikiwanyonya badala ya kuwakwamua na
wimbi kubwa la umasikini.









Ameyasema hayo jana tarehe 01/08/2017 wakati
akizungumza na wakulima wadau wa kilimo Mifugo na Uvuvi na wananchi kwa ujumla
wakati wa uzinduzi wa sikukuu ya wakulima – nane nane, Maonesho yenye kauli
mbiu ya “Zalisha kwa Tija Mazao na
Bidhaa za Kilimo Mifugo na Uvuvi ili kufikia Uchumi wa Kati”
yanayofanyika Kitaifa kwenye uwanja
wa maonesho ya kilimo wa Ngongo Mkoani Lindi.









Alisema
kuwa kutokana na malalamiko hayo Rais wa Jamhuri ya muungano wa Tanzania Mhe
Dkt John Pombe Magufuli aliamua kufuta baadhi ya kodi na tozo katika sekta
ndogondogo za mazao ili kuibua tija ya uwajibikaji na ukuzaji wa uchumi.









Alisema Jumla ya tozo 80 kati ya tozo 139 zimefutwa
na tozo nne (4) zimepunguzwa viwango. Tozo, kodi na ada zinajumuisha  kufutwa kwa tozo kumi (10) na mbili (2)
kupunguza viwango kwenye zao la tumbaku.
Kwenye zao la kahawa zimefutwa tozo 17 na moja (1) kupunguzwa kiwango;
sukari zimefutwa 16; pamba tozo zilizofutwa ni mbili (2); kwenye korosho tozo
mbili zimefutwa na chai imefutwa tozo moja (1).









Katika kuongeza upatikanaji wa pembejeo tozo tatu (3) zimefutwa na
moja (1) imepunguzwa kiwango kwenye mbolea na
tozo saba (7) zilizokuwa kwenye mbegu nazo zimefutwa. Katika Ushirika
jumla ya tozo 20 zimefutwa katika ngazi mbalimbali.









Alisema
kuwa
katika Mifugo; kodi, ada na
tozo saba (7) ambazo zilikuwa kero kwa Wafugaji, Wafanyabiashara na Wawekezaji
nazo zilifutwa na kubakiza zile tu zenye uhusiano wa moja kwa moja katika
uendelezaji wa Sekta ya Mifugo. Tozo zilizofutwa zinajumuisha mbili (2) kwenye
maziwa; nyama tozo nne (4) na moja (1) kwenye afya ya mifugo.  









Katika Uvuvi, jumla ya kodi, ada na tozo tano (5) ambazo ni kero
kwa Wavuvi, Wafugaji wa viumbe kwenye maji na wawekezaji nazo zimefutwa.









Alisema kuwa Serikali itaendelea kuchambua kwa kina tozo, ushuru
na ada mbalimbali zilizobaki katika kilimo, mifugo na uvuvi kwa lengo la
kuangalia uhalali wa kuwepo kwake ili kuwapunguzia wakulima, wafugaji na wavuvi
mzigo wa tozo, ushuru na ada zisizokuwa na tija.









‘‘Serikali pia imechukua hatua za makusudi kupunguza ushuru wa mazao
uliokuwa unatozwa na Serikali za mitaa kutoka asilimia 5 hadi asilimia 3  kwa mazao ya biashara na kufikia asilimia 2
kwa mazao ya chakula. Vile vile, Serikali imezielekeza Serikali za Mitaa kuacha
kutoza ushuru kwa wazao yanayosafirishwa halmashauri moja kwenda Halmashauri
nyingine yenye uzito usiozidi tani moja (1)
’’ Alisema Mhe Nasha









Aliongeza kuwa Hatua nyingine iliyochukuliwa ni ya kusamehe kodi
ya ongezeko la thamani kwenye vyakula vya mifugo vinavyotengenezwa hapa nchini
ili kupunguza gharama ya kununua chakula hicho kwa Wafugaji. Serikali pia,
imesamehe kodi ya ongezeko la thamani kwenye mayai ya kutotoleshea vifaranga,
lengo likiwa ni kupunguza gharama ya uzalishaji vifaranga na kukuza Sekta ndogo
ya Ufugaji ili iweze kuongeza mchango katika Pato la Taifa.









Mhe
Nasha alisema kuwa Kuanzia msimu huu wa
kilimo Wakulima wa korosho watapata bure pembejeo aina ya salfa zilizokuwa
zikiuzwa kwa bei ya ruzuku.









Hatua hiyo ya utekelezaji wa azma ya Serikali ya Awamu ya Tano
ni  kuhakikisha kuwa vikwazo vyote
vilivyokuwa vinawakabili wakulima wa
zao la korosho vinaondolewa ili waongeze uzalishaji na tija zaidi kutokana na
zao hilo.









Aidha alisema kuwa Serikali itaendelea
kuhimiza matumizi ya Mfumo wa Stakabadhi Ghalani. Mfumo huu umesaidia kupanda
kwa bei ya korosho na mapato kwa wakulima kupitia vyama vikuu vya ushirika vya
TANECU, MAMCU, RUNALI, Lindi Mwambao, TAMCU na CORECU. 









Alisema wakulima na wafanyabiashara Wote ni
mashahidi kuwa katika msimu wa ununuzi uliopita wa mwaka 2016/2017 vyama hivyo
viliuza korosho na kuwalipa wakulima jumla ya Shilingi bilioni 809.18
ikilinganishwa na malipo ya Shilingi bilioni 293.09 msimu wa 2015/2016. Kiasi
hiki cha fedha ni kikubwa na ni mafanikio makubwa ambayo ni ya kujivunia.









MWISHO