Msemaji wa rais wa zamani wa Zimbabwe Robert Mugabe amesema alikuwa na wasiwasi kwamba raia nchini humo "wangemburura na kumuua" kiongozi huyo kama ilivyotokea nchini Libya.

Wakati wa wiki ya mwisho madarakani, Bw Mugabe alikuwa amewekwa kwenye kizuizi kwake nyumbani baada ya jeshi kuchukua udhibiti wa serikali.
Baadaye aliondolewa kikamilifu kutoka madarakani.
"Nilianza kufikiria picha sawa na za Muammar Gaddafi," George Charamba, ambaye ni msemaji wa zamani wa Bw Mugabe amesema.
Alikuwa anazungumza na tovuti ya kibinafsi nchini Zimbabwe ya Daily News.
Huku akikumbuka siku za mwisho za utawala wa Mugabe wa miaka 37, Charamba anasema kiongozi huyo wa miaka 93 alitaka kuondoka madarakani "kwa masharti yake" na kwamba alikuwa ametahadharishwa kuhusu hatari iliyokuwepo baada ya jeshi kuchukua udhibiti wa nchi na maandamano kuzuka.
Mugabe alipokuwa anazuiliwa katika makao yake ya kifahari ya Blue Roof mazungumzo kuhusu mustakabali wake yalikuwa yanafanyika kati ya majenerali, makasisi wa kanisa Katoliki, wasaidizi wake wa kisiasa na wajumbe kutoka Afrika Kusini.
Bw Charamba anasema maafisa wa jeshi waliwafahamisha kwamba maelfu ya waandamanaji waliokuwa wanamtaka Mugabe angejiuzulu, kulikuwa na uwezekano, wangetaka kumfikia Mugabe binafsi.
"Ingewezekana kwa sababu wanajeshi hao walitwambia 'hatuwezi kuwafyatulia risasi raia ambao wanaandamana dhidi ya rais na kummwaga damu," Charamba amenukuliwa na tovuti ya Daily News.
Kiongozi wa zamani wa Libya Muammar Gaddafi alikamatwa na kisha kuuawa mwaka 2011 baada ya maandamano na maasi ambayo yalifikisha kikomo utawala wake wa miongo minne.