FARU Ndugai, mnyama aliyepewa jina la Spika wa Bunge la Jamhuri ya Tanzania, Job Ndugai, ndiye hasa alikuwa kivutio kwa wabunge katika Kamati ya Bunge ya Kudumu ya Ardhi, Maliasili na Mazingira waliotembelea Hifadhi mseto ya Ngorongoro, ingawa hawakufanikiwa kumuona faru huyo.
Kutomuona kwao, wabunge hao waliambulia kumuona faru mwingine maarufu kwa kuwa na umri mkubwa kuliko wote, yaaniBibi Fausta (55) ambaye kwa sasa amejengewa banda maalum ili kumhifadhi kutokana na faru Fausta kuwa hana tena nguvu za kujilinda katika kutafuta malisho ndani ya bonde kuu la Ngorongoro ambalo limesheheni maelfu ya wanyama wakali wakiwemo simba, chui, mbwa mwitu na fisi (wapatao 500) ambao ni rahisi kumshambulia mnyama yeyote mnyonge.
Faru Ndugai ambaye hivi sasa kashika nafasi ya ‘Faru John,’ kwa kuwa ndiye mnyama mkali zaidi Ngorongoro na mwenye kupenda kuzua rabsha ndani ya kreta, aliripotiwa kuwa alikuwa amekwenda ‘kutalii,’ sehemu nyingine ya hifadhi hiyo, kama ilivyo kawaida yake.
“Huwa kiusalama hatutakiwi kutaja idadi ya wanyama adimu kama Faru ambao huwindwa sana kwa pembe zao, lakini inatosha kusema kuwa kwa sasa Bonde la Ngorongoro ndilo sehemu pekee yenye faru wengi nchini Tanzania,” alisema Mhifadhi wa Ngorongoro, Dakta Fred Manongi. Tanzania ina zaidi ya Faru 110 huku idadi ya wanyama hao waliobaki duniani kwa sasa ikiwa ni takriban Faru 5,000 tu.
Nchi za Kenya, Namibia, Zimbabwe, Afrika Kusini na Tanzania zinamiliki asilimia 98 ya faru wote weusi waliopo duniani Kuhusu Faru Ndugai, Dk Manongi alieleza kuwa mnyama huyo anayebeba jina la Spika wa Bunge, hawezi kuonekana kwa urahisi bondeni humo, maana mara nyingi ni mzururaji anayependa kuzurura huku na kule na ni mkorofi.
“Hivi karibuni Faru Ndugai aliua ng’ombe wawili alipotoka nje ya kreta,” alifafanua Dk Manongi na kuongeza kuwa, kutokana na mazingira hatarishi wanapoishi faru, wanyama hao wamejenga tabia ya kujihami na kitu chochote ambacho watakiona kuwa ni kigeni na kutishia usalama wao. Mbunge wa Geita, Joseph Kasheku ‘Musukuma’ (CCM) na Mbunge wa Arumeru Mashariki, Joshua Nassari (Chadema) walitaka kufahamu jinsi Faru Ndugai alivyoweza kupewa jina la Spika.
Manongi alieleza kuwa kwanza Faru huyo alizaliwa wakati Spika Ndugai alikuwa mjumbe wa Bodi ya Mamlaka hiyo na pili kiongozi huyo wa Bunge ni mhifadhi wa kudumu nchini. Hata hivyo, uongozi wa hifadhi ya Ngorongoro umetangaza kuwa utaratibu wa kuwapa majina Faru na wanyama wengine muhimu uko mbioni, kuandaliwa na mara utakapokamilika, basi kutakuwa na sherehe maalum ya uzinduzi.
Wajumbe hao wa Kamati ya Ardhi, Maliasili na Mazingira, akiwemo Katibu Mkuu wa Wizara ya Maliasili na Utalii, Meja Jenerali Gaudence Milanzi walitembelea Makumbusho makubwa ya Zamadam yaliyopo eneo la Olduvai Gorge ndani ya hifadhi hiyo ya Ngorongoro.
|
0 Comments