SERIKALI imesema, itaendelea kuzifungia nyimbo zinazokiuka maadili ya Mtanzania na kwamba, jambo hilo ni la kawaida duniani kote.
Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Dk. Harrison Mwakyembe amesema bungeni mjini Dodoma kuwa, si wasanii wa Tanzania tu wanaofungiwa nyimbo zao na kwamba, uamuzi huo una lengo la kulinda maadili.

Waziri Mwakyembe amelieleza Bunge kuwa, Serikali imewasamehe wasanii ambao nyimbo zao zilifungiwa, wasirudie tena kutoa nyimbo zinazokiuka maadili ya Mtanzania.
"Yanayotokea Tanzania yanatokea duniani kote ....maana viongozi wetu hapa wanalalamika ni kwa sababu dunia pana hawajaielewa. Davido mwanamuziki maarufu duniani ambaye amepiga na kijana wetu Diamond (Nassib Abdul ) hapa kafungiwa nyimbo zake mbili na Nigeria Broadcasting Corporation mwaka huu" amesema Waziri Mwakyembe wakati anajibu swali la nyongeza la Mbunge wa Viti Maalum, Catherine Magige.
Mbunge huyo aliuliza kwa nini Serikali inazifungia nyimbo za wasanii baada ya kupigwa kwa muda mrefu kwenye jamii, na kwamba, si kwamba kamati ya maudhui ya Baraza la Sanaa la Taifa (BASATA) imeshindwa kazi?
"Sio huyo tu, Wiz Kid kafungiwa nyimbo zake, 9ice kafungiwa nyimbo zake, sijasikia wabunge wa Nigeria wakilalamikia sheria zao wenyewe, sisi wabunge kazi yetu kubwa ni kuheshimu, kuhakikisha jamii inaheshimu, inalinda sheria za nchi, na tutaendelea...Koffie Olomide amepiga wimbo unaitwa Ekotite, umepigwa marufuku kupigwa Congo DRC, waheshimiwa wabunge mnaoenda Congo, ikienda uwaambie wakupigie Ekokite watakushangaa, huo wimbo ni matusi, sisi wabunge tunakuwa wa kwanza kuruhusu nchi yetu iwe kokoro" amesema Waziri Mwakyembe.
Ametoa mfano mwingine kuwa, miezi michache iliyopita mwanamuziki Rick Ross ambaye ameshirikiana na mwanamuziki Mtanzania, Nassib Abdul kutoa wimbo wa Wakawaka amepata matatizo Marekani kwa kutoa wimbo ambao maudhui yake yanatoa picha kwamba anaunga mkono ubakaji.
"Mheshimiwa Naibu Spika, BBC ambayo ipo Uingereza, ambako ndugu zangu ndio mwanzo wa ustaarabu, wamefungia nyimbo 237 katika historia yao, sisi hapa tunalalamika nyimbo mbili kufungiwa, tutaendelea kufungia kulinda utamadunia wa nchi yetu" amesema. Kwa mujibu wa Waziri Mwakyembe, wanawake nchini humo waliandamana, wimbo ukaondolewa kwenye televisheni zote, na kijana huyo akaomba radhi.
"Kwa Tanzania sisi tumekuwa kokoro kwamba tupokee kila kitu kwa sababu hatuna utamaduni, Baba wa Taifa Mheshimiwa Naibu Spika alisema mwaka 1962 Taifa lisilo na utamaduni wake ni Taifa mfu, na sisi hatuwezi kukubali kuwa Taifa mfu"amesema.
Amelieleza Bunge kuwa, kuna mmomonyoko mkubwa wa maadili nchini hivyo Serikali lazima ichukue hatua ikiwa ni pamoja na kuzifungia nyimbo zisizo na maadili.