Mahakama Kuu ya Tanzania, imeidhinisha uamuzi wa msajili wa vyama vya kisiasa Tanzania kumtambua Profesa Ibrahim Lipumba kuwa mwenyekiti halali wa chama cha CUF.
Hukumu hiyo imetolewa na Jaji Benhajj Masoud katika mahakama kuu kanda ya Dar es Salaam wakati akizitaka pande zote mbili kukaa meza moja kwa majadiliano.

Ni kesi ambayo kambi ya Maalim Seif Sharif Hamad ndani ya chama hicho walifungua mahakamani kupinga msajili wa vyama vya siasa kumtambua Lipumba baada ya kujiuzulu na kurudi kwenye chama mnamo 2016.
Kumekuwepo mvutano ndani ya chama CUF baada ya Prof Lipumba kuwasilisha barua ya kujiuzulu kama mwenyekiti mwaka 2015 lakini akarejea tena wakati chama kilipokuwa kinajiandaa kumchagua mwenyekiti mpya.
Lipumba alijiuzulu kupinga uteuzi wa Edward Lowassa kuwa mgombea wa uraisi wa muungano wa vyama vya upinzani uliyofahamika kama Ukawa katika uchaguzi mkuu wa Tanzania mwaka 2015.

Mabadiliko ndani ya CUF

Mwishoni mwa Juma Chama cha Wananchi (CUF) kimemchagua Khalifa Suleiman Khalifa kuwa katibu mkuu wake mpya kufuatia uchaguzi uliofanywa na baraza kuu la chama hicho.
Mwenyekiti wa CUF, Profesa Ibrahim Lipumba amemtangaza Khalifa ambaye ni mbunge wa zamani wa Gando kuchukua nafasi ya Maalim Seif Sharif Hamad Jumamosi katika makao makuu ya CUF jijini Dar es Salaam.
Wengine waliyochaguliwa na Magdalena Sakaya ambaye sasa ni naibu katibu mkuu bara huku Fakhi Suleiman Khatibu akichaguliwa naibu katibu mkuu upande wa Zanzibar.
Ndani ya chama cha CUF makundi yote mawili ya Maalim Seif (Pichani) na Profesa Lipumba yanachukuliwa kuwa na nguvu za aina yake,
Image captionNdani ya chama cha CUF makundi yote mawili ya Maalim Seif (Pichani) na Profesa Lipumba yanachukuliwa kuwa na nguvu za aina yake,
Mabadiliko hayo yanakuja licha ya mgogoro wa uongozi ambao umefanya chama hicho kumeguka huku Bwana Hamad akiongoza mrengo mmoja na Profesa Lipumba akiongoza mrengo mwingine.
''Makundi yote mawili ya Maalim Seif na Profesa Lipumba yanachukuliwa kuwa na nguvu za aina yake, hali ambayo imekuwa ikikiteteresha chama hicho kadiri ya siku zinavyokwenda.'' anasema Markus Mpangala, mchambuzi wa siasa nchini Tanzania.
Mgogoro wa sasa unaingia katika awamu nyingine ambapo wanachama na wafuasi wamegawanyika katika pande hizo mbili, huku wakiwa katikati ya giza nene kuelekea katika uchaguzi Mkuu wa mwaka 2020 visiwani Zanzibar na Tanzania Bara.
Swali kuu wachambuzi wanahoji katika mazingira haya, Je hatua zinazoshuhudiwa zitasaidia kwa kiasi gani kukiinusha daraja chama hicho cha upinzani katika siasa Tanzania