Bondia wa uzani wa juu kutoka nchini Marekani Deontay Wilder ameshindwa kuficha hisia zake juu ya pambano la leo alfajiri ambapo bondia Anthony Joshua alinyukwa na Andy Ruiz Jr.
Ulimwengu wa masumbwi kwa muda sasa umekuwa na shauku kubwa ya kushuhudia pambano baina ya Wilder na Joshua ambaye ni Mwingereza mwenye asili ya Nigeria.
Pambano hilo la mabondia hao wawili ambao mpaka jana wote walikuwa hawajawahi kupigwa limekuwa likipigiwa upatu kama mpambano mkali zaidi wa ndondi za uzani wa juu kuwahi kutokea katika miaka ya hivi karibuni.
Hata hivyo, Wilder mara kadhaa amekuwa akimtuhumu Joshua kwa kuzuia pambano hilo kwa kutengeneza vikwazo lukuki ili wasikutane ulingoni.
Kutokana na tuhuma hizo, haishangazi namna ambavyo Wilder amepokea matokeo ya ushindi wa Ruiz Jr dhidi ya Joshua.
Kupitia ukurasa wake wa twitter, Wilder maarufu kama Bronza Bomber ameandika: "Hakuwa bingwa wa kweli. Maisha yake yote ya ndondi yalikuwa yametawaliwa na uongo, kujichanganya na zawadi. Sasa tunajua ni nani ambaye alikuwa anamkimbia mwenzake."
Katika pambano hilo lilopigwa jijini New York, Joshua alilambishwa sakafu mara nne na Ruiz Jr kabla ya mwamuzi kuvunja pambano katika raundi ya saba.
Kwa ushindi huo, Ruiz ambaye hakupigiwa upatu kabla ya pambano amemvua Joshua mikanda mitatu ya ubingwa wa WBA, WBO na IBF.
Pambano hilo ni la kwanza kwa Joshua kupigwa, ameshinda mapambano yote 22 kabla.
Kilichompata Joshua kinalinganishwa na kilichowakumba mabingwa wa zamani Lennox Lewis na Mike Tyson ambao pia waliwahi kupigwa na wapinzani ambao hawakupigiwa upatu na kuzua mshangao mkubwa kwenye ulimwengu wa masumbwi.
Tyson alitandikwa na James 'Buster' Douglas mwaka 1990, na Lewis alichapwa na Hasim Rahman mwaka 2001.
Tyson Fury 'ampoza' Joshua
Bondia mwengine anayewekwa kwenye mizani sawa ya ubora na makali na Wilder na Joshua kwa sasa ni Tyson Fury.
Wilder na Fury walizichapa Disemba Mosi 2018, japo pambano hilo liliisha kwa sare, wachambuzi wengi wanaamini Fury alinyimwa ushindi wa wazi.
Fury ambaye pia ni raia wa Uingereza hajaonesha kusherehekea kupigwa kwa Joshua.
Badala yake amemtumia salamu kupitia ukurasa wake wa Twitter akimwambia vitu kama hivyo (kupigwa) ni vya kawaida na amemtaka kunyanyuka na kujipanga upya.
Promota wa Joshua Eddie Hearn ametangaza kuwa bondia wake atarejeana na Ruiz kabla ya mwaka kuisha kwenye mwezi Novemba ama Disemba jijini London.
Hearn amebainisha kwa kwa sasa mazungumzo yoyote ya kuzipiga dhidi ya Fury ama hata Wilder yamesitishwa.
|
0 Comments