Waziri wa biashara wa Kenya Peter Munya amekana shutuma za kupanga mauaji ya Naibu Rais William Ruto, vyombo vya habari nchini humo vimeripoti.

Waziri Munya alikuwa akizungumza nje ya makao makuu ya ofisi ya Mkurugenzi wa uchunguzi wa makosa ya jinai (DCI) ambako aliitwa , sambamba na mawaziri wengine, kuhojiwa kuhusu shutuma kuwa walimtishia bwana Ruto, Gazeti la the Standard limeripoti.
Wameshutumiwa kufanya vikao vya siri,the Standard limeongeza, lakini bwana Munya amewaambia waandishi wa habari kuwa hawajapeleka taarifa polisi kwa kuwa bwana Ruto hajapeleka malalamiko rasmi.

Peter Munya, Waziri wa teknolojia ya mawasiliano Joe Mucheru na waziri wa masuala ya vijana Sicily Kariuki waliwasili kwenye ofisi za DCI baada ya kuitwa kwa ajili ya mahojiano sambamba na Katibu Mkuu wa wizara ya nishati na mafuta Andrew Kamau, na Joseph Njoroge wa wizara ya nishati.
Waziri Munya amekiri kuwa kulikuwa na mikutano lakini ''haikuwa mikutano ya mipango ya kumuua naibu rais,''Bwana Munya, alisema.
Daily Nation la Kenya lilimnukuu waziri akisema kuwa Naibu Rais Ruto alidai kuwa mawaziri hao walikuwa wakifanya vikao vya siri na maafisa wengine.
Naibu Rais Ruto ana mipango ya kuwania urais mwaka 2022.