Tete Kafunja alikwenda kutoa dhamana kwa rafiki yake aliyekamtwa kwa kosa la kuuza bangi, baada ya kufika hapo alikamatwa na kupewa kesi ya mauaji.
Kabla ya hapo Tete alikua akiendesha biashara ya kuuza vinywaji vya pombe maarufu kama Bar maeneo ya Manzese Jijini Dar Es salaam. Alikua na mke na mtoto mmoja.
Baada ya kukamatwa alikaa gereza la keko jijini Dar es salaam kwa miaka 11 kama mahabusu akisubiri hukumu yake.
Mnamo 2003 alihukumiwa kunyongwa, lakini akakata rufaa dhidi ya kuhumu hiyo kutokana na kigezo alichowasilisha kuwa kesi haikuwa na ukweli.
''Baada tu ya hukumu, nilikata rufaa maana sijawahi hata kuiona sura ya marehemu, sijui chochote mimi nilienda kumuwekea dhamana rafiki yangu aliyekua amekamatwa kwa kosa la kukutwa na bangi, nikashangaa na mimi nakamatwa kisa sijui nini, baadae ndio nikaambiwa nina kesi ya kuua mtu jambo ambalo ni la kushangaza na sijawahi hata kumuona huyo marehemu'' amesema Tete.
Maisha Gerezani wakati wa kusubiri Kunyongwa
Tete anasema baada ya kuhukumiwa alikua akisubiri kunyongwa. Maisha yalikua magumu sana na walipewa jina maalum la 'vipusa' kwa maana watu wanaolindwa na wanasubiri kufa tu.
''Kwa wafungwa wa kunyongwa, maisha ni magumu sana, unakaa ndani tuu, na kutoka ni mara moja moja wakati wa kuota jua, unaletewa uji asubuhi lakini hata hamu ya kunywa uji hakuna''
Baada ya kukata rufaa Tete aliambiwa anatakiwa kuhamishiwa katika gereza la Isanga Dodoma. Tayari kwa kunyongwa ikiwa raisi atatoa idhini wanyongwe, hata kama kesi imekatiwa rufaa.
Rufaa na kuachiwa Huru
Baada ya kukamatwa mwaka 1990, alikaa kama mahabusu kwa miaka 11, kisha akahukumiwa kunyongwa.
Mwaka 2008 kesi yake ya rufaa ilisikilizwa kwa mara ya kwanza katika mahakama ya rufaa Jijini Dar es salaam, na ikawa inasikilizwa taratibu, mwaka 2008 mwishoni hatimaye akakutwa hana hatia na kuachiliwa Huru.
''Wakati jaji anasema unaachiliwa huru, sikuamini kabisa, nikauliza tena nimeachiwa huru? Wakasema ndio ikabidi sasa nirudishwe jela baada ya kibali kutoka nikaachiliwa rasmi, sikuamini niliomba sana Mungu na kumshukuru kwa maajabu yaliyotekea.
Mara baada ya kuachiwa Tete alikabidhiwa kiasi cha Shilingi Elfu moja tu ya kitanzania sawa na nusu dola ya Marekani, kisha akaambiwa aondoke.
Maisha ya Uraiani kwa mara ya kwanza
Mara baada ya kuachiwa Tete alifunga safari hadi eneo la Kimara jijini Dar es saalam, alishangaa sana kuona jinsi mji ulivyobadilika na kuona magari mengi, jambo ambalo ni geni kwake. Akaitafuta sana familia yake lakini akaambiwa walihama na hawajulikani walienda wapi, mke wake na mtoto mmoja.
Kuna mzee mmoja jirani yake ndio mtu pekee alikua akimfahamu.
''Nikamwambia mimi ni Tete, akakataa akesema Tete yupo gerezani na inawezekana hivi sasa ameshanyongwa, nikamwambia hapana, ni mimi akasema hebu nione mwanya, Tete ninayemjua ana mwanya, baada ya kumuonesha ndo akaniamini, nikaanza kumuelezea kisa kizima''
Hadi sasa Tete haijui familia wala ndugu zake wako wapi, wote walikata tamaa na wakadhani ameshanyongwa. Amewatafuta sana bila mafanikio yoyote.
Ana mtazamo upi juu ya hukumu ya kunyogwa?
Kwa mujibu wa sheria za Tanzania, baada ya mahakama kumtia mtu hatiani na kumsomea adhabu ya kunyongwa mpaka kifo, mamlaka ya kutekelezwa adhabu hiyo inabidi kwanza ipate ridhaa ya kiongozi mkuu wa nchi, tena kwa kutia saini.
Takriban wafungwa 500 katika jela za Tanzania wanakabiliwa na hukumu hiyo. Rais wa Tanzania, John Magufuli amekwisha weka wazi msimamo wake juu ya utekelezaji wa hukumu ya kifo. Hawezi kusaini mfungwa yeyote aliyehukumiwa adhabu hiyo kwenda kunyongwa.
Mara ya mwisho kwa mfungwa kunyongwa nchini ilikuwa mwaka 1994, enzi za utawala wa Rais wa awamu ya pili wa nchi hiyo, Ally Hassan Mwinyi.
Tete anasema hukumu hii ni mbaya sana na ifutwe ili wasiwatese wafungwa ambao hawajui hatma yao.
''Unateseka na kama hujafanya kosa kama mimi si wote wanaokata rufaa na kufanikiwa, kuna watu wengi nimewaacha jela, hata sura za marehemu hawazijui. Nadhani ifutwe, maisha yangu yameharibika sana na sijalipwa fidia yoyote, sina familia wala ndugu''
Hii leo Mahakama ya Tanzania inatarajiwa kutoa uamuzi juu ya hukumu ya kifo iwapo inafaa kutekelezwa au la.
Wanaharakati wa haki za kibinadamu waliwasilisha madai wakisema kuwa hukumu hiyo inakiuka haki za kibinadamu za kuishi kama ilivyo katika katiba ya taifa hilo.
0 Comments