MWAKA jana mshindi wa Taji la Miss Kinondoni alikuwa ni Queen Elizabeth Makune ambaye alivuka moja kwa moja hadi kuibuka mshindi wa Miss Tanzania na kuiwakilisha vyema nchi yetu Miss World.
Leo hii ndani ya Viwanja vya Life Park, Mwenge jijini Dar es Salaam kutawaka moto kwa warembo 18 wakiwania nafasi ya kumrithi Queen Elizabeth katika Shindano la Miss Kinondoni 2019.
TUJIUNGE KAMBINI
Tangu kuanza kwa maandalizi ya shindano hili, washiriki wote 18 wameshafanya mengi kwa kushirikiana ambapo wiki mbili zilizopita walikula chakula cha pamoja na watoto yatima wa Kituo cha Malaika, Mwananyamala jijini Dar.
Licha ya kula nao chakula cha pamoja, washiriki hao walijumuika pamoja katika zoezi la kuosha magari ya wadau mbalimbali wa mashindano hayo ambapo kwa gari moja walikuwa wakiosha kuanzia shilingi 10,000 na kuendelea.
Katika siku hiyo, walifanikiwa kukusanya jumla ya shilingi 500,000 ambazo waliwapatia wahusika wa kituo hicho kwa ajili ya mahitaji mbalimbali ya watoto.
MISS TALENT
Mapema wiki hii, ndani ya Viwanja vya Life Park, warembo hao walijumuika pamoja katika kushindana kuonesha vipaji (telents) vyao.
Miongoni mwa vipaji walivyoonesha ni kuimba, kucheza, kuigiza na kuchora.
Akizungumza na MIKITO kuhusiana na mshindi, mratibu wa shindano hilo, Nancy Joseph alisema kwamba mshindi atatajwa leo (Jumamosi) kabla ya kumpata mshindi wa Miss Kinondoni.
“Mshindi wa Miss Talent tunatarajia kumtangaza Jumamosi (leo) kwa hiyo wote walioshiriki walifanya vizuri na mwisho wa siku mshindi mmoja atapatikana,” alisema Nancy.
ZAWADI
Hadi sasa zawadi kubwa ya mshindi wa kwanza imeshajulikana ambayo ni gari ndogo la kisasa aina ya Mini Cooper lenye thamani ya shilingi milioni 18.
“Mshindi wa pili atapata seti ya bedroom (samani ya chumbani) huku zawadi kwa mshindi wa tatu ikiwa ni TV ya kisasa (flat screen inchi 43) ambapo zawadi hizi zitatolewa na wadhamini.
“Mshindi wa nne na kuendelea watapata zawadi ndogo ndogo zikiwemo kompyuta mpakato (laptop),” alimaliza kusema Nancy.
VIINGILIO
Kiingilio katika shindano hilo kitakuwa shilingi 10,000 kawaida, 20,000 VIP na kwa meza yenye watu 10 ni 300,000.
MDHAMINI MKUU
Miss Kinondoni 2019 imedhaminiwa na radio janja kiganjani mwako +255 Global Radio. Jinsi ya kuipata ingia www. globalradio. co.tz au pakua APP katika Playstore kwenye simu yako ya mkononi kwa kuandika 255 global radio.
0 Comments