Mjumbe wa Kamati ya Habari,machapisho na utangazaji wa Kamati Kuu ya maandalizi ya mkutano wa SADC Eshe Muhidin akitoa mrejesho wa mjadala wa siku ya kwanza wa semina ya waandishi wa habari kwa ajili ya kuwajengea uwezo kwa ajili ya kuripoti mkutano wa SADC unaotarajia kufanyika  Agosti mwaka huu
 Baadhi ya waandishi wa habari wakifutilia Mafunzo yanayohusu kuandika habari  zenye weledi katika mkutano wa SADC unaotarajia kufanyika Agosti mwaka huu
 Mwandishi Hafidh Kido akifuatilia mjadala katika semina ya waandishi wa habari inayoendelea mkoani Morogoro ambayo inayohusu kuwajengea uwezo waandishi wa habari kuhusu mkutano wa SADC
 Mjumbe wa Kamati ya Habari ,machapisho na utangazaji wa Kamati kuu ya maandalizi ya mkutano wa SADC Nelly Mtema akifuatilia mjadala wa semina ya kuwajengea uwezo wandishi wa habari katika kuandika habari zinazohusu mkutano wa SADC
 Do.Kanael Kaale ambaye ni moja ya wanafunzi(katikati) katika semina ya kuwajengea uwezo waandishi wa habari nchini Tanzania ikiwa ni maandalizi ya kuelekea mkutano wa SADC
 Mshiriki wa semina ya waandishi wa habari inayolenga kuwajengea uwezo wa kuandika habari za SADC ,Abdallah Majura akisikiliza mada kutoka kwa watoa mada(hayupo pichani) .Semina hiyo inafanyika mkoani Morogoro
 Naibu Mkurugenzi wa Idara ya Habari (MAELEZO) Zamarad Kawawa akijadiliana jambo na mmoja wa wajumbe wa kamati ya maandalizi ya mkutano wa SADC unaotarajia kufanyika Agosti mwaka nchini Tanzania
 Sehemu ya washiriki wa semina  inayohusu kuwajengea uwezo waandishi wa habari nchini ili kuwawezesha kuandika habari za mkutano wa Jumuiya ya Maendeleo ya Nchi za Kusini barani Afrika (SADC) unaotarajia kufanyika Agosti mwaka huu



WAKATI Rais wa Tanzania Dk. John Magufuli, akitarajiwa kukabidhiwa uenyekiti wa nchi 16 zilizopo kwenye Jumuiya ya Maendeleo ya Nchi za Kusini mwa Afrika (SADC), wachambuzi wabobezi kuhusu jumuiya hiyo wamesema, wakuu wa nchi hizo na serikali zao wana matumaini makubwa na Rais Magufuli.

Hii ni kutokana na mambo makubwa aliyoyafanya kwa Tanzania ndani ya muda mfupi, hadi kuonekana ni nchi mfano katika sekta mtambuka za maendeleo.

Aidha, matumaini makubwa yapo kwenye usimamizi wa rasilimali za Afrika ili kumudu kujitawala kiuchumi na kiuongozi dhidi ya mataifa yanayoendelea au nchi wahisani.Hayo, yameelezwa kwenye semina ya siku tatu ya waandishi wa habari inayoendelea mkoani Morogoro kwa awamu ya pili, ambapo watoa mada ni wabobezi katika masuala ya mtangamano wa jumuiya mbalimbali zilizoundwa barani Afrika.

Semina hiyo, inayolenga kuwapa mwanga wanahabari kuhusiana na masuala ya SADC, ikiwa ni mkakati wa kuwaandaa kuelekea mkutano mkubwa wa jumuiya hiyo utakaofanyika Agosti mwaka huu.

Mtoa mada kwenye semina hiyo Katibu Mkuu mstaafu Mussa Uledi alisema, katika mkutano huo wa SADC pamoja na mambo mengine nchi ya Tanzania itaingia kwenye historia kwani mkutano huo utatumika kumkabidhi kijiti Rais Dk. Magufuli cha kuwa Mwenyekiti wa jumuiya hiyo kwa kipindi cha mwaka mmoja.

"Nchi za zilizomo kwenye SADC kwanza zinatambua nafasi ya Tanzania kwenye jumuiya hiyo na mchango wake mkubwa katika ukombozi wa nchi za Kusini mwa Bara la Afrika."Ukweli uliopo Rais Dk. Magufuli atakabidhiwa Uenyekiti wa SADC na tunafahamu miongoni mwa malengo ya jumuiya hiyo ni kuimarisha uchumi wa nchi hizo na Bara la Afrika kupitia uchumi wa viwanda."

Amesema, katika eneo la viwanda nchi mbalimbali za Afrika zimeona namna ambavyo Rais Magufuli amesimama imara kuhakikisha ujenzi wa viwanda nchini Tanzania unafanyika, na hivyo ukitazama kwa kina utabaini kuwa nchi za SADC zina matumaini makubwa na Rais Magufuli.

"Maono ya jumuiya hiyo yanakwenda sambamba kabisa na maono ya ya Rais wetu ambaye amesimama imara kuimarisha uchumi wa nchi yetu ya Tanzania na mpango wake ni kuona Tanzania inafikia uchumi wa kati kupitia viwanda," alisema.

Amesema, kikubwa kinachosubiriwa kwa Rais Magufuli ni mtindo wake wa uongozi na kusimamia mambo yakamilike kwa wakati badala ya kuendeleza utamaduni wa kuzungumza na kuacha mambo kwenye nyaraka.

kwa upande wake, Mkurugenzi wa Shirika la Utangazaji Tanzania (TBC), Dk. Ayoub Rioba wakati akiwasilisha mada yake alisema anashangaa wanahabari hawaandiki ipasavyo namna Rais Magufuli alivyofanya mambo makubwa ndani ya muda mfupi wa uongozi wake.

Ameongeza kuwa haijawahi kutokea hata kwa kiongozi wa kiafrika kujipambanua kama mtu asiyeshidwa na kuaminisha wananchi kuwa Afrika si masikini."Zaidi ya mara moja Rais Magufuli alishasema Tanzania si nchi masikini, kwa pamoja tunaweza kuwa nchi watoa misaada badala ya kuendelea kupokea misaada kutoka nchi zilizoendelea," alisema Dk. Rioba na kuongeza:

"Kuna mambo makubwa katika sekta ya madini, afya, miundombinu na bandari bila kusahau usafirishaji. Yote hii inaongeza hamu kwa nchi wanachama wa SADC, kutaka kuona maendeleo haya yanakwenda katika jumuiya hiyo."

Kingine kilichogusiwa ni namna kiongozi huyo alipogusia umuhimu wa lugha ya Kiswahili kuzungumzwa katika nchi zote za Afrika na dunia.Vilevile, katika mkutano huo wa SADC ambao unafanyika mara ya pili nchini tangu ulipofanyika kwa mara ya kwanza mwaka 2003, kutakuwa na kipengele cha kujadili matumizi ya lugha ya Kiswahili katika shughuli mbalimbali za jumuiya.

Hadi sasa, tayari nchi kadhaa za kusini mwa Afrika zimeomba kupelekewa walimu na vifaa vya kufundishia lugha ya Kiswahili ikiwemo Zimbabwe, Afrika Kusini na Namibia.