Mhe Hakimu (aliyeketi mbele) akisikiliza kesi ndani ya Mahakama inayotembea mkoani Mwanza.
Gari likiwa eneo linapopaki Buhongwa Mwanza mnamo Agosti 22, 2019.
Baadhi ya wananchi wakisubiri huduma eneo la Buhongwa jijini Mwanza.


Jumla ya Mashauri 14 yamefunguliwa na kusikilizwa na Mahakama inayotembea ‘mobile court’ mkoani Mwanza.

Kwa mujibu wa Mkurugenzi wa Menejimenti ya Usimamizi wa Mashauri-Mahakama ya Tanzania, Mhe. Eva Nkya amesema kuwa mashauri hayo yamefunguliwa na kutolewa maamuzi katika kipindi cha mwezi Julai, 2019.

Mhe. Nkya alieleza kuwa Mahakama hiyo inayotembea inaendelea kutoa huduma katika maeneo mbalimbali mkoani Mwanza huku Mahakama nyingine inayotembea iliyopo jijini Dar es Salaam inaendelea kutoa elimu kwa Wadau juu ya uendeshaji wa Mahakama hiyo.

Kwa mkoa wa Mwanza, Mahakama hiyo inafanya kazi katika maeneo ya Igoma, Buswelu na Buhongwa na kwa upande wa Dar es Salaam Mahakama hiyo inatoa huduma katika maeneo ya Bunju ‘ A’, Kibamba, Buza na Chanika.

Mkurugenzi huyo aliongeza kuwa Mahakama inayotembea inasikiliza mashauri yote  yanayosikilizwa  na Mahakama  za Mwanzo  kama vile migogoro ya ndoa, madai, mirathi na jinai, pamoja na rufaa  kutoka Mabaraza ya kata, yakiwemo mashauri yanayojitokeza katika operesheni maalmu zinazofanywa na taasisi/vyombo mbalimbali  vya serikali.

Huduma nyingine zitolewazo na Mahakama hiyo ni kutoa taarifa za mashauri, kutoa fomu za viapo na kuthibitisha nyaraka mbalimbali, kufanya usuluhishi kwa wadawa na kutoa elimu kuhusiana na masuala ya Mahakama.

Mnamo Februari 06, 2019, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli alizindua rasmi Mahakama inayotembea lengo likiwa ni kusogeza huduma kwa wananchi na kutoa haki kwa wakati.

Aidha; lengo jingine ni kuwapunguzia wananchi gharama za kufuata huduma za Mahakama mbali na maeneo wanayoishi.

Mahakama ya Tanzania ina mpango wa kutanua wigo wa utoaji huduma hii kwa kuanzisha vituo vingine katika mikoa iliyosalia kwa awamu tofauti.


Na Mary Gwera, Mahakama