WAKATI Tanasha Donna akisubiri kujifungua mtoto wa kiume muda wowote kuanzia sasa, aliyekuwa mpenzi wa mwandani wake, Nasibu Abdul ‘Diamond Platnumz’, Zarinah Hassan ‘Zari The Boss Lady’ amerusha mawe kama kawaida yake na kumtahadharisha mama kichacho huyo. 


Ikumbukwe kuwa, Zari kabla ya kumwagana na Diamond au Mondi, alijaliwa kupata watoto wawili ambao sasa anawalea mwenyewe hivyo amempa onyo hilo Tanasha ambaye ndiye mpenzi wa sasa wa Mondi ili ajiandae kisaikolojia na asifikiri furaha aliyonayo sasa itadumu.

VITISHO VYENYEWE…
Zari aliyeishi kwenye uhusiano na Mondi kwa takriban miaka mitano kabla ya kuachana, amekaririwa na mtandao maarufu wa habari za mastaa nchini Kenya akisema hana kinyongo na ex-wake (Mondi), lakini anampa onyo Tanasha awe makini.
Zari alisema, Tanasha anaweza kuona kwa sasa Mondi ana ‘kiraruraru’ cha kupata mtoto na kuonesha mapenzi, lakini jamaa huyo anaweza kubadilika muda wowote kwani ameshayafanya hayo kwa wanawake wengine waliotangulia akiwemo mwanamitindo Hamisa Mobeto.

“Kupetiwapetiwa katika kipindi hiki ni kitu kizuri, lakini anatakiwa kuwa macho sana. Anatakiwa kuangalia msururu wa warembo waliomtangulia pamoja na mimi, sioni kitu kipya kwa Nasibu (Mondi), naona ni yuleyule,” alikaririwa Zari katika mtandao huo.

WANANZENGO WAMKOSOA ZARI
Maoni mbalimbali yaliyotolewa na mashabiki kwenye mtandao huo, watu walimkosoa Zari kwa kumtaka aachane na Tanasha kwani yeye wakati wake umeshapita na anapomzungumzia inaonekana ni dhahiri anateswa na wivu. “Huu ni wivu tu unamtesa, si akae kimya?

Anamzungumzia Tanasha ili iweje huyu Tukinao (Zari)?” Maoni ya aina hiyo yalitawala kwenye mtandao huo na mingine mingi iliyosambaza habari hiyo.

MONDI VIPI?
Kwa upande wake Mondi licha ya kusikia kauli hizo mara kwa mara kutoka kwa Zari, imeelezwa kuwa ameamua kukaa kimya kwani anachoamini kinachomsumbua Zari kwa sasa ni wivu na anaona kumjibu ni kupoteza muda.
“Mondi ameshamfuatilia Zari kwa muda mrefu, anaonekana anasumbuliwa na wivu tu, siyo kitu kingine, ndiyo maana kutwa haishi kumzungumzia Mondi au Tanasha, sasa ameamua tu kukaa kimya kwani amempuuza tu na yeye sasa hivi yuko bize na maisha yake mapya,” alisema mtu wa karibu na familia ya Mondi ambaye hakupenda jina lichorwe gazetini.

Gazeti la Ijumaa Wikienda lilimtafuta Mondi kuhusiana na ishu hiyo mwishoni mwa wiki iliyopita katika pati ya baby shower ya Tanasha, hakutaka kuizungumzia zaidi ya kile kilichowapeleka siku hiyo (baby shower) katika Hoteli ya Best Western Coral Beach iliyopo Masaki jijini Dar.

TUJIKUMBUSHE
Zari ambaye ni mama wa watoto watano, alimwagana na Mondi Februari 14, mwaka jana ambapo kila mmoja alichukua hamsini zake. Mondi alijitosa kwa Tanasha, lakini Zari yeye ameuaminisha umma wa wapenda ubuyu kuwa kwa sasa ana mume aitwaye King Bae ingawa hajawahi kumfichua sura yake mitandaoni.