Mamlaka nchini Canada zimekamata ndege ya Tanzania aina ya Bombardier Q400.
Hii ni mara ya pili kwa ndege ya nchi hiyo kuzuiliwa nchini Canada.
Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Prof. Palamagamba Kabudi amethibitisha kukamatwa kwa ndege hiyo iliyokuwa iwasili nchini hivi karibuni.
Sababu ya kukamatwa kwa ndege hiyo, kwa mujibu wa Prof Kabudi ni kesi iliyofunguliwa na mkulima mstaafu raia wa Namibia Hermanus Steyn.
Steyn pia alifungua kesi nchini Afrika Kusini mwezi Agust iliyosababisha ndege aina ya Air Bus 220-300 izuiliwe na hatimaye serikali ya Tanzania kushinda kesi mahakamani
"Mhe. Rais ndege yetu aina ya Bombadier ambayo ilipaswa ifike Tanzania kutokea Canada imekamatwa na mtu yule yule ambaye aliikamata ndege yetu kule Afrika ya Kusini." - Prof. Palamagamba Kabudi, ailisema mjini Dodoma katika hafla ya kuapishwa kwa mabalozi.
Steyn, anadai fidia ya dola milioni 33 baada ya mali zake kutaifishwa na Serikali ya Tanzania mwaka 1980.
Hata hivyo, Septemba 3, 2019 mahakama hiyo iliamuru ndege hiyo iliyokuwa imezuiwa katika uwanja wa ndege wa Oliver Tambo kuachiwa baada ya Serikali kushinda kesi bila kutoa fedha yoyote.
Maelezo zaidi
Profesa Kabudi amesema kuendelea kwa vitendo hivyo ni hujuma za mabeberu wasiofurahishwa na maendeleo nchini.Katika hafla hiyo iliyohudhuriwa na Rais wa Tanzania, John Magufuli aliyewaapisha mabalozi hao, Profesa Kabudi alisema,.
"Tulikwenda mahakamani tukamshinda (Afrika Kusini) akakata rufaa na wiki iliyopita tukamshinda tena, huyohuyo sasa amekimbilia Canada amekamata ndege ya Bombardier Q400 ambayo ilikuwa ifike nchini.""Jambo linalosikitisha ndege zilizokuwa zinatoka Marekani aina ya Dreamliner mbili hazikukamatwa zimefika lakini kila ndege inapotakiwa kuondoka Canada tunashangaa hao matapeli wanajuaje na ndege zinakamatwa."
Tanzania yaeleza hasira zake kwa Canada
Amesema Balozi wa Tanzania nchini Canada aliitwa nchini na kuelezwa jinsi nchi isivyofurahishwa na kukamatwa kwa ndege zake kila zinapokaribia kuja kuondoka nchini humo."Nimemwambia sio tu kwamba tunasikitika bali tunakasirishwa, na tunafikiri mheshimiwa rais kukushauri kama Canada inaendelea kuruhusu vitu kama hivyo sio wao peke yao wanaotengeneza ndege, hatukufanya makosa kununua ndege Canada, hata Brazil wanatengeneza ndege," amesema Profesa Kabudi.Amesema wameandaliwa wanasheria kwenda Canada kuipigania ndege hiyo.
Kushikiliwa kwa ndege hiyo kunarejesha kumbukumbu ya ndege nyingine ya Tanzania aina ya Bombardier Q400-8 iliyozuiwa nchini Canada mwaka 2017 kutokana na madai ya Sh87.3 bilioni zilizokuwa zikidaiwa na kampuni ya kikandarasi.
Mkulima anayesababisha kukamatwa kwa ndege za Tanzania ni nani?
Mkulima Hermanus Steyn ni Mtanzania mwenye asili ya Afrika Kusini ambaye pia alipigwa marufuku kukanyaga nchini Tanzania.
Amekuwa akiidai serikali ya Tanzania zaidi ya $30 million kutokana na madai ya tangu miaka ya 1980 ambapo serikali ya Tanzania ilipoingia katika sera ya utaifishaji na kuchukua mali nyingi zilizokuwa za watu binafsi na mashirika mbali
Kwa mkulima huyu, inadaia kuwa serikali ilichukua shamba kubwa la mbegu lililokuwa likifahamika kama Rift Valey Seed Company lililokuwa mjini Arusha.
Vitu vingine vya mkulima huyu ambavyo serikali inadaiwa kuvitaifisha ni pamoja na vifaa vya ukulima, mifugo, majengo, magari 250 na ndege ndogo 12
Baada ya kufanya mashtaka, miaka ya 1990, mahakama iliamuru alipwe $33 million kama fidia.
Mnamo tarehe 4 May 1985, bwana Steyn alijulishwa kiasi cha fedha atakacholipwa kama fidia. Siku tisa baadaye, Steyn alikubali kupokea taarifa hiyo lakini hauthibitisha kwamba amekikubali kiwango cha fidia hiyo.
Lakini kwa mujibu wa baadhi ya taarifa, serikali ya Tanzania ilimlipa $20m pekee.
Wakili wa Steyn ameviambia vyombo vya habari kwamba kufuatia miaka mingi kupita bila kukamilishwa kwa deni hilo, kiasi cha $16 milioni kilichobaki kimeendelea kuongezeka kwa riba hadi kufikia tena $33 milioni.
|
0 Comments