PASI na shaka, mzazi mwenza wa staa wa Bongo Fleva, Nasibu Abdul ‘Diamond Platnumz’, Zarinah Hassan ‘Zari The Boss Lady’ anazidi kuthibitisha kwamba ni mwanamke mtata.
Kinachoendelea kwa sasa ni kwamba, mwanamama huyo anadaiwa kuanzisha vita upya na Diamond au Mondi.
MIAKA MIWILI YA KUACHANA
Wawili hao wiki hii wanatimiza miaka miwili tangu Zari alipotangaza rasmi kuachana na Mondi Siku ya Wapendanao (Valentine’s Day) Februari 14, 2018 wakiwa wamejaaliwa watoto wawili, Tiffah Dangote na Nillan.
Mwanamama huyo ambaye ni mjasiriamali wa nchini Uganda mwenye makazi Durban, Afrika Kusini anadaiwa kuanza tena chokochoko na Mondi.
Kupitia ukurasa wa Instagram wa mwanaye Tiffah Dangote, Zari ameweka video za watoto wa Mondi wakionekana kuwa na midomo mikubwa.
ETI WAMERITHI
Wambeya wa mitandaoni wanajua kuwa Mondi amekuwa akikejeliwa na mahasimu wake kutokana na mdomo wake mkubwa.
Zari ambaye ni mama wa watoto watano aliposti video hiyo ikiwaonesha Tiffah na Nillan na kuweka ‘emoji’ ya mdomo mkubwa kisha kumjibu mmoja wa watu walioiona video kuwa hiyo ndiyo nembo ya familia yao.
Zari alikwenda mbele zaidi na kuandika; “Tusizungumzie mdomo mkubwa, wameridhi, ipo kwenye vinasaba (DNA)”
Pamoja na kwamba, jambo hilo limefanyika kwenye ukurasa wa Tiffah, lakini wanaojua mambo kwa undani wanaeleza kwamba ukurasa huo wenye wafuasi milioni 2.4 unaendeshwa na Zari mwenyewe.
BADO ZARI ANA HANGOVER?
Baadhi ya mashabiki walioamini kuwa Zari alishakata tamaa kwa Mondi walidai kuwa, bado mwanamama huyo ana ‘hangover’ ya penzi la jamaa huyo.
“Baada ya kuwa na huyo King Bae kidogo alitulia, lakini nasikia ameachana naye ndiyo maana ameanza tena vurugu zake,” ilisomeka sehemu ya maoni ya mashabiki wa Mondi juu ya ishu hiyo aliyoifanya Zari.
AMESHINDWA ‘KU-MOVE ON’?
Mwingine alisema; “Mtu umezaa naye watoto wawili, kutwa unamdhalilisha kwenye mitandao ya kijamii, hii inaonesha wazi kwamba Zari ameshindwa kabisa ku-move on (kuendelea na maisha baada ya kuachana na Mondi)”
MWENDELEZO WA MASHAMBULIZI
Kabla ya kuirejesha vita hiyo mwaka huu, mwaka jana mashambulizi yalikuwa ni bandika bandua ambapo Zari aliwatumia watoto hao kwa mara nyingine kumtukanisha Mondi kwenye mitandao.
Zari aliwafananisha watoto hao na vitoto vya kima akimlenga Mondi.
Kama hiyo haitoshi, Zari alitumia mahojiano maalum kumshambulia Mondi kwa kusema kwamba ametelekeza watoto wake na kwamba ni mwanaume suruali.
Mbali na hilo, Zari alidai kuwa, alimwacha Mondi kwa sababu ni ‘womanizer’ (anapenda kubadilisha wanawake).
Kwa upande wake, Mondi alijibu pigo moja tu, kwamba aliamua kuachana na Zari kwa sababu alimsaliti na staa wa muziki wa Nigeria, Peter wa P-Square.
MADHARA KWA WATOTO
Vita hii ya Zari kuwatumia watoto kumdhalilisha baba yao, Mondi ina madhara makubwa ya kisaikolojia ya muda mfupi na ya muda mrefu yanayoweza kuwapata watoto hao.
Tafiti zinaonesha kuwa watoto huwa hawana ulinzi wowote wa kisaikolojia wa kuchuja, migogoro hiyo huwajengea uoga unaotokana na kuhofia watakachofanya wazazi.
Uhusiano kati ya wazazi na watoto huathirika, watoto huanza kujenga msongo wa mawazo taratibu ambao utaathiri afya zao ya kiakili na kimwili.
Mwaka 2012 wataalam wa saikolojia na mambo ya kijamii walifanya utafiti uliochapishwa kwenye Jarida la Child Development ambapo watafiti walitumia taarifa walizozikusanya kwenye familia 235 za kipato cha kati na cha juu.
Waliwahoji wazazi wa watoto ambao walikuwa wanasoma shule za awali, wakati watoto wao wakiwa shuleni. Waliwauliza mmojammoja kuhusu maisha yao na kama walikuwa na migogoro kati yao na kwa kiwango gani.
Miaka saba baadaye, wakati watoto wakiwa na umri mkubwa, walirejea kwenye familia hizo na kuwahoji wazazi pamoja na watoto kwa nyakati tofauti. Waliulizwa kuhusu migogoro ya wazazi, tabia na mienendo yao na kuwafuatilia watoto hao kwa siku kadhaa.
Utafiti huo ulibaini kuwa watoto ambao wazazi wao walikuwa na migogoro mikubwa au walikuwa wakigombana mara kwa mara, walikuwa wakipatwa na msongo na kuwa na uwezekano wa kupata sonona, kuwa na uoga pamoja na tabia nyingine hatari kwa afya ya akili na mwili.
Utafiti mwingine uliofanywa mwaka 2013 na kuchapichwa kwenye jarida hilo ulibaini kuwa watoto ambao wazazi wao walikuwa na migogoro walipata athari kubwa katika uwezo wao wa kutatua matatizo kwa haraka na kufikiri (cognitive performance).
Migogoro ya wazazi inaweza kumsababishia mtoto matatizo ya uwezo wa kula vizuri yanayofahamika kitaalam kama anorexia.
Wataalam wanaeleza kuwa mtoto anayetoka kwenye familia yenye migogoro mikubwa ana hatari ya kujiingiza kwenye tabia za uvutaji sigara, ulevi na hata matumizi ya mihadarati.
Kama wazazi wanagombana, inaweza kuathiri uwezo wa watoto kiakili
0 Comments