Aliyekuwa Mbunge wa Ndanda (Chadema), Cecil Mwambe
Mbunge wa Ndanda (Chadema), Cecil Mwambe amejiuzulu uanachama wa chama hicho kikuu cha upinzani nchini Tanzania na kujiunga na CCM leo Jumamosi Februari 15, 2020.
Mwambe ambaye takribani miezi miwili iliyopita alijitosa kugombea uenyekiti wa Chadema akichuana na mwenyekiti wa chama hicho, Freeman Mbowe ametangaza uamuzi huo mbele ya katibu wa itikadi na uenezi wa CCM,
Humphrey Polepole. Katika uchaguzi huo Mwambe alishindwa na Mbowe.

 
Akizungumza kuhusu uamuzi wake huo Mwambe amesema vyama vya upinzani nchini vina safari ndefu ya kujenga demokrasia ya kweli, ameona atakuwa anajidanganya na kuwadanganya wapiga kura wake kubaki katika vyama vya namna hiyo wakati bado anatamani kuwatumikia wananchi wa Ndanda.

“Leo kwa kuamua mwenyewe nimeamua kujiunga na CCM kama mtanipokea na kunikaribisha basi nipewe tena nafasi ya kugombea endapo mtaridhia na nitapata nafasi,” amesema Mwambe.

Mwambe ambaye alijiunga Chadema mwaka 2015 akitokea CCM ambako jina lake lilikatwa katika mchakato wa kura ya maoni kuwania kupitishwa kugombea ubunge, amesema ndani ya Chadema hakuna uwazi katika suala la mapato na matumizi na wanachama hawana nafasi ya kuhoji lakini wanaonufaika ni wachache.

Paia amesema uamuzi wake wa kugombea uenyekiti na Mbowe uliibua chuki na laianza kuandamwa.