DAR: Mwenyekiti wa Chama cha ACT- Wazalendo, Maalim Seif Shariff Hamadi amesema kutokana na misingi aliyoijenga kwa wafuasi wake visiwani Zanzibar, amefanikiwa kukipindua Chama cha Wananchi (CUF) visiwani humo kwa asilimia 100.
Pia amesema licha ya kuwepo kwa changamoto mbalimbali kuelekea uchaguzi mkuu wa mwaka huu, ACT-Wazalendo hakitasusia uchaguzi huo.
Maalim Seif ametoa kauli hiyo juzi wakati akizungumza na wahariri wa Kampuni ya Global Publishers baada ya kufanya ziara katika Ofisi za kampuni hiyo zilizopo Sinza-Mori jijini Dar.
Alisema kabla ya Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Dar kukubaliana na uamuzi wa Msajili wa Vyama vya Siasa kumtambua Profesa Ibrahim Lipumba kuwa Mwenyekiti halali wa CUF, Maalim Seif pamoja na wafuasi wake walikuwa wameshafanya utafiti na kufahamu hatima yao kisiasa.
“Tuliunda kamati tukawaambia wapitie katika vyama washiriki wa Ukawa ili kuwauliza endapo watatupokea na vyama vyote vilisema vitatupokea, ila waliokuwa wepesi zaidi ni ACT-Wazalendo ndiyo maana mahakama ilipoamua saa sita mchana sisi saa nane tukatangaza kwenda huko yaani ‘Shusha tanga pandisha tanga’,” alisema.
Alisema baada ya kuhamia ACT-Wazalendo, asilimia kubwa ya waliokuwa wafuasi wa CUF nao pia walihamia ACT jambo ambalo linamhakikisha kuufuta ufalme wa CUF Zanzibar.
“Kwa mfano wapo wanaosema tulivamia na kuchukua ofisi za matawi wakati si kweli, ni kwamba CUF ilikuwa na majengo mawili inayoyamiliki Mtendeni na Kilimahewa, mengine yote ni nyumba za watu binafsi ambao wao walitupatia nyumba zao kwa imani yao kwa CUF baada ya kuondoa wakabadili misimamo, kwamba ulipo Maalim na sisi tupo.
“Kwa hiyo hatujaenda huko kwa bahati mbaya, ukishajiunga kwenye chama hiki baada ya wiki moja unaweza kugombea nafasi yoyote na tumeendana vizuri kabisa kwa sababu nimeshinda kwa asilimia 97 ya kura. Ado Shaibu ambaye ni katibu mkuu kijana kabisa kapata asilimia 100 ya kura zake. Kwa hiyo uongozi ni mchanganyiko wa zamani na wapya,” alisema.
Alisema kutokana na mikakati hiyo wanaamini kuwa ACT-Wazalendo itashinda uchaguzi mkuu wa Zanzibar kwa kishindo.
“Naamini tutashinda kwa sababu kabla ya sisi na wenzangu kutoka CUF, ACT-Wazalendo ilikuwa na matawi machache sana, lakini sasa hivi Zanzibar imebadilika na kuwa purple, CUF ukitafuta hukioni tena na sitafanya kazi tena na Profesa Lipumba, ” alisema.
…MUDA WA MABADILIKO YA TUME BADO UPO
Aidha, alisema licha ya kwamba baadhi ya watu wanadai muda wa kuibadilisha Tume ya Taifa ya uchaguzi kuwa tume huru hautoshi, si kweli kwa sababu muda upo wa kutosha.
“Kinachotakiwa ni kupelekea muswada wa sheria bungeni kwa hati ya dharura, tena CCM wenye wabunge wengi wanaweza kupewa maelekezo tu kuupitisha muswada huo, kwa hiyo suala la muda kuwa mdogo hatulikubaliani nalo.
“Ila hata kama hatukupata tume huru hatususii uchaguzi, sisi ni kujipanga tu kwenye uchaguzi huu. Tumemaliza chaguzi zetu ndani ya chama kazi kubwa ni kushinda uchaguzi mkuu,” alisema.
Pamoja na mambo mengine alisema muungano wa vyama vya upinzani kuelekea uchaguzi mkuu kama ilivyokuwa kwa Ukawa mwaka 2015, bado upo.
“Niseme kwamba kuna utashi kwenye vyama, kwamba tuzungumze ili tuweze kukubaliana tujifunze makosa ili yasijirudie tena,” alisema.
….HUKUMU CHADEMA
Akizungumzia hukumu ya viongozi wa Chadema walihukumiwa kifungo miezi mitano jela au kulipa faini milioni 350 kwa wote, mwenyekiti huyo mpya wa ACT alisema anahisi viongozi hao walionewa.
“Kwanza sipendi kuingilia mahakama, ni chombo huru, lakini kiubinadamu nahisi ni maonevu makubwa. Mwanasiasa siyo mfanyabiashara, hata pesa ya kula hana, halafu unamwambia alipe shilingi milioni 10 kila kosa.
“Shilingi milioni 350 jumla wa chini milioni 30 juu milioni 70, mahakama lazima iangalie hukumu inazotoa, huwezi kuifanya mahakama kama TRA kukusanya mapato. Lile suala ni kama hakimu aliteleza kidogo,” alisema Maalim Seif.
Aidha alisema licha ya Lipumba kumkaribisha ndani ya CUF, hana mpango wa kupata naye.
“Sitapana na Lipumba kabisa kwa sababu ni msaliti, siwezi kufanya naye kazi, ila nitakuwa nasalimiana naye kama kawaida,” alisema.
Kwa picha za ziara ya Maalim Seif ndani ya Global, funua ukurasa wa 14.
Stori: GABRIEL MUSHI, Ijumaa
0 Comments