MFANYABIASHARA maarufu kwa sasa kwa upande wa wasanii Bongo Muvi, Faiza Ally, ambaye pia ni ‘baby mama’ wa mbunge wa Mbeya mjini Joseph Mbilinyi ‘Sugu’, amewafunga midomo mastaa wa Bongo Muvi kwa kuporomosha mjengo wa hatari.


Akizungumza na AMANI, Faiza alisema kuwa hakuna kitu kizuri kama jitihada kwenye maisha ya kila siku.
“Nyumba ambayo mnaiona kwenye mitandao niliwahi kuiposti wanangu wapo hapo iko Dodoma, ni yangu na niliijenga kwa nguvu zangu unazoziona nahangaika kila kukicha, lakini nimenunua kiwanja kandokando ya bahari kabisa huko Kigamboni,” alisema Faiza.

Mwanamama huyo ambaye ni kama ameipa kisogo sanaa, alisema ameona hakuna njia zaidi ya kuchakarika na kutafuta maisha kwani mambo yanaenda tofauti sana kwa hivi sasa, hivyo anatengeneza maisha kwa ajili ya wanawe.

“Sijui nisemaje, jamani hakuna kitu kizuri kama jitihada maishani, nilikuwa natamani hivi ambavyo ninavyo hivi sasa na kweli Mungu amenipa na anaendelea kunipa lakini ningejibweteka sidhani kama ningepata hivi vyote,” alisema Faiza ambaye anaonekana wazi kuwaacha mbali kabisa mastaa mbalimbali wa Bongo Muvi kwa jitihada anazozifanya.

Mastaa wengi Bongo Muvi hususan wa kike hawana nyumba zaidi huishi nyumba za kupanga.