Rais wa Tanzania John Pombe Magufuli leo Jumapili Mei 3 amesema atatuma ndege Madagascar kwenda kufuata dawa ya mitishamba ambayo rais wa nchi hiyo anadai kuwa inatibu corona.
Magufuli amesema kuwa amewasiliana na Madagascar baada ya kupokea barua rasmi kutoka nchi hiyo iliyoeleza kuwa wamegundua dawa ya corona.
"Ninawasiliana na Madagascar na wameshaandika barua. Wanasema kuna dawa zimepatikana kule, tutatuma ndege kule na dawa zile zitaletwa pia ili Watanzania nao waweze kufaidika nayo… Sisi serikali tupo tunafanya kazi usiku na mchana."
Rais Magufuli ameyasema hayo hii leo katika hafla fupi ya kumwapisha Mwigulu Nchemba kuwa Waziri wa Katiba na Sheria akichukua nafasi iliyoachwa wazi na Balozi Augustine Mahiga aliyefariki Ijuumaa.
Hata hivyo, shirika la Afya Duniani (WHO) limeonya juu ya ubora wa dawa hiyo ambayo ni kinywaji kilichotengenezwa kwa mitishamba.
Matunda, ndege, mbuzi wakutwa na corona
Wakati huo huo, rais Magufuli amesema pia sampuli kadhaa ambazo hazikuwa za binadamu zilitumwa katika maabara ya taifa hilo ili kupima ubora na usahihi wa majibu ya mashine hizo katika vipimo vya ugonjwa huo.
''Sampuli hizo zilipewa majina ya binadamu na kupelekwa bila ya wataalamu wa maabara kujua kuwa si za bidanamu'', ameeleza Magufuli.
Sampuli ya oili ya gari ilipewa jina la Jabiri Hamza na haikukutwa na corona. Sampuli ya Tunda la fenesi ilipewa jina la Sara Samuel majibu yake hayakukamilika, sampuli ya papai iliitwa Elizabeth na kukutwa na corona.
Sampuli ya ndege kwale pia ilikutwa na corona pamoja na mbuzi pia.
"…Lazima ugundue kuna mambo ya ajabu yanafanyika nchi hii. Ama wahusika wa maabara wamenunuliwa na mabeberu, ama hawana utaalamu jambo ambalo si kweli kwa kuwa maabara hii imetumika sana katika magonjwa mengine. Ama zile sampuli zinazoletwa maana vifaa vyote vinatoka nje, hivyo lazima kuna kitu fulani kinafanywa," amesema Magufuli.
Magufuli amesema kutokana na taarifa hizo anaamini kuna watu ambao walipewa majibu yasiyo sahihi.
"Lazima kuna watu wameambiwa positive lakini si wagonjwa wa corona, na inawezekana wengine wakafa kwa hofu. Papai lile lipo halijafa linaiva tu. Mbuzi yule yupo tu hajafa, fenesi lile lipo tu labda lije kuoza…kwa hiyo natoa wito kwa Watanzania msiwe na hofu…mbona mafua yamekuwepo lakini haya ni makali, nayo yatapita..."
Kutokana na hilo, Magufuli amemwagiza waziri Nchemba kwenda kufanya uchunguzi katika maabara hiyo na endapo kutakuwa na jambo lolote la jinai litakalogundulika basi hatua zichukuliwe.
Magufuli pia ametaka uchunguzi zaidi kwa nchi za Afrika na WHO juu ya sampuli na ubora wa vifaa vya kupimia maradhi hayo.
Kuhusu wanyama kukutwa na corona, nchini Marekani paka wa kufugwa nyumbani, simba na chui wa kufugwa kwenye mabustani pia wamekutwa na virusi hivyo.
Waliofunga makanisa na misikiti washutumiwa
Magufuli pia ameshutumu vyombo vya habari vya kimataifa kwa namna vinavyoripoti kuhusu janga hilo nchini Tanzania licha ya kuwa vipo katika maeneo ambayo yaneathirika zaidi.Pia amewashutumu viongozi wa dini ambao wamefunga nyumba za ibada na kuwasifu wale wanaoendelea na ibada misikitini na makanisani katika kipindi hiki. Kuhusu wapinzani kususia vikao vya Bunge Dodoma amesema ameshatoa maelekezo kuwa wasilipwe posho zao na kuwatuhumu kwa kutumiwa na mabeberu. Katika hatua nyengine, rais Magufuli amesema anafikiria kuruhusu ligi ya mpira iendelee hata kwa kuoneshwa kwenye runinga na anasubiria ushauri wa wataalamu wake kabla ya kulifanyia uamuzi jambo hilo.
Matamshi yake yanajiri baada ya rais wa Madagascar Andry Rajoelina kutangaza kwamba taifa lake limezindua dawa ya mitishamba ya kutibu Covid-19.
0 Comments