Rais wa Tanzania John Pombe Magufuli ametetea nafasi yake baada ya kushinda kwa kishindo Uchaguzi Mkuu uliofanyika Jumatano wiki hii.
Magufuli ameshinda kwa kupata kura 12,516,252 ambayo ni asilimia 84 ya kura zote zilizopigwa.
Tundu Lissu kutoka chama cha upinzani cha Chadema ameshika nafasi ya pili kwa kupata kura 1,933,271 ya kura zote ziizopigwa.
Jumla ya watu 15,91950 walipiga kura hizo wakati waliojiandikisha kupiga kura walikuwa 29,754,699 kwa mujibu wa Tume ya taifa ya Uchaguzi (NEC).
"John Magufuli ndio mshindi wa uchaguzi , amepata kura nyingi halali kuliko wagombea wengine, amechaguliwa kuwa rais wa tanzania na Samia suluhu Hassan kuwa makamu wa rais,''Mwenyekiti wa Tume ya uchaguzi Jaji Semistocles Kaijage ametangaza.
Ni rasmi sasa mgombea wa chama tawala nchini Tanzania CCM, John Pombe Magufuli amechaguliwa tena kwa ushindi wa kishindo.
Vyama vikuu vya upinzani hata hivyo tayari walishakataa matokeo ya uchaguzi wa siku ya Jumatano wakidai uligubikwa na udanganyifu.
Uchaguzi huu ambao Magufuli alikuwa akiwania nafasi hiyo ya juu alikuwa na washindani wengine 14.
Siku ya Alhamisi, Bwana Lissu alisema hayakubali matokeo akisema kuwa ''uchaguzi huo haukufuata sheria za Tanzania na za kimataifa''.
Alidai kuwepo kwa masanduku ya ''kura feki'' .
Pia alidai kuwa mawakala wa chama chake walizuiwa kuingia kwenye vituo vya kupiga kura wakati wa kura za Jumatano.
Mwenyekiti wa tume ya uchaguzi Semistocles Kaijage alisema madai hayo hayana msingi wowote.
Rais wa zamani wa Burundi Silvestre Ntibantunganya ambaye ndiye Mwenyekiti wa ujumbe wa waangalizi wa uchaguzi kutoka Afrika Mashariki, amesema kuwa uchaguzi mkuu Tanzania ulifanyika kwa kufuata taratibu.
Ujumbe huo umetoa wito kwa vyama vya kisiasa kufuata taratibu za kisheria katika kuwasilisha madai yao.
Ubalozi wa Marekani nchini Tanzania umesema kuwa tuhuma za upinzani zina msingi.
0 Comments