Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mwanza, Jumanne Muliro akizungumza na waandishi wa habari jana kuhusiana nahali ya usalama kabla na baada matokeo ya uchaguzi mkuu.

WATU sita wamekamatwa wilayani Ukerewe wakidaiwa kuchoma nyaraka mbalimbali za ofisi ya Afisa Mtendaji wa Kata ya Kagunguli.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mwanza, Jumanne Muliro alithibitisha kukamatwa kwa watuhumiwa hao jana wakati akizungumza na waandishi wa habari mara baada ya kuulizwa na gazeti hili kuhusu tukio hilo.

Alisema watu sita bila kuwataja majina, wanashikiliwa na jeshi la polisi wilayani Ukerewe kwa tuhuma za kuvunja mlango wa jengo la ofisi ya Afisa Mtendaji wa Kata ya Kagunguli na kuchoma nyaraka mbalimbali za ofisi hiyo.

“Watuhumiwa hao walikamatwa baada ya kuchoma karatasi (nyaraka) mbalimbali kwenye ofisi hiyo ya Mtendaji wa Kata kwa hisia kuwa kulikuwa na karatasi za ziada za kupigia kura,kabla ya kufanya tukio hilo walivunja mlango wa jengo hilo lenye ofisi sita,”alisema Muliro. Alisema kuwa jeshi la polisi linaendelea na uchunguzi wa tukio hilo utakapokamilika litawafikisha mahakamani kwa mujibu wa sheria ili kujibu tuhuma zinazowakabili..