TIMU ya Taifa Tanzania ya Tanzania jana imepoteza kwa kufungwa bao 1-0 kwenye mchezo wa kirafiki dhidi ya Burundi uliochezwa Uwanja wa Mkapa.

Kwenye mchezo wa jana ambao mgeni rasmi alikuwa ni Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa kipindi cha kwanza timu zote mbili zilitoshana nguvu baada ya kwenda vyumba vya kubadilishia nguo wakiwa hawajafungana.

Kipindi cha pili mambo yalizidi kuwa magumu kwa timu zote mbili ambapo Stars ilijaribu kufanya mashambulizi yalishindwa kuzaa matunda na Burundi ilikuwa ya kwanza kupiga shuti la kwanza ambalo lililenga lango kipindi cha pili.

Bao pekee la ushindi lilipatikana dakika ya 84 kupitia kwa Said Ntibazonkiza na kuwafanya Burundi kuibuka na ushindi ugenini.

Simon Msuva nyota wa timu ya Taifa ya Tanzania, Taifa Stars amesema kuwa haikuwa bahati kwao kwa kuwa walipambana ili kupata ushindi ila mambo yalikuwa magumu kwao.

Stars ilimaliza dakika 90 ikiwa pungufu baada ya kiungo mkabaji Jonas Mkude kuonyeshwa kadi nyekundu dakika ya 78 kwa kuwa alikuwa alionyeshwa kadi mbili za njano.