ff

CHANZO CHA PICHA,GETTY IMAGES

Maelezo ya picha,

Waziri mkuu wa Tanzania, Kassim Majaliwa

Wadau wa siasa, vikiwemo vyama vya upinzani nchini Tanzania wanakutana kwa siku tatu mjini Dodoma. Mkutano huo wa siku tatu utakaoanza Oktoba 21-23 mwaka huu, utahudhuriwa na Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa, pamoja na viongozi wengine wa serikali wakiwemo baadhi ya mawaziri.

Akithibitisha hilo, Msajili msaidizi wa vyama vya siasa nchini Tanzania, Sixty Nyahoza ameiambia BBC kwamba, mbali na waziri mkuu na baadhi ya mawaziri, mkutano huo utahusisha pia wadau wote muhimu katika siasa vikiwemo vyama vya siasa, Azaki, waandishi wa habari na viongozi wa dini.

Kwa mujibu wa Katiba na sheria za Tanzania, Waziri mkuu ni msimamizi wa shughuli zote za serikali katika Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, ikiwemo ndani ya bunge, lenye mamlaka ya kutunga na kurekebisha sheria mbalimbali za nchi.

Alipoulizwa na BBC kuhusu ajenda kubwa ya mkutano huo, Sixty alisema 'ni kujadili maudhui ya utekelezaji wa sheria zinazoratibu shughuli zote za siasa Tanzania'.

Mkutano huo unakuja kufuatia kuwepo kwa mvutano wa muda mrefu kuhusu kuzuiwa kwa shughuli za kisiasa nchini humo, ambapo vyama vya upinzani vimekuwa vikilalamika kunyimwa fursa ya kufanya mikutano ya kisiasa kama sheria zinavyotaka.

qqq

CHANZO CHA PICHA,THECITIZEN

Maelezo ya picha,

Msajili msaidizi wa vyama vya Siasa Tanzania, Sisty Nyahoza

Awali msajili wa vyama vya siasa nchini humo aliitisha kikao cha pamoja kati ya Jeshi la Polisi na vyama vya siasa, lakini baadhi ya vyama vikiwemo vikubwa vya upinzani kama CHADEMA na ACT-Wazalendo, viligomea mkutano huo vikitaka mkutano huo muhimu uhusishe pia watu wenye wajibu wa kisiasa akiwemo Waziri Mkuu na mawaziri wenye dhamana za kisiasa.

'Kuzuiwa' kwa mikutano ya kisiasa

Shughuli za siasa, ikiwemo mikutano ya hadhara ya kisiasa, mikutano ya ndani na maandamano ni haki ya raia kwa mujibu wa katiba ya Tanzania.

Lakini alipoingia madarakani kupitia uchaguzi mkuu wa mwaka 2015, aliyekuwa rais wa awamu ya tano wa Tanzania, hayati John Magufuli alinukuliwa akisema shughuli za siasa ikiwa ni pamoja na maandamano na mikutano ya hadhara isimame hadi uchaguzi mkuu wa mwaka 2020. Alisema uchaguzi umepita iopita, "sasa ni wakati wa kazi tu".

Kwa upinzani hilo lilionekana kama zuio kwao, ingawa Mamlaka za serikali haziwahi kuthibitisha kuzuia, zaidi ya kusema mikutano ya ndani ya vyama inafanyika na wabunge wnaa madiwani wanaendeleea na mikutano katika maeneo yao ya uchaguzi.

Kwa sababu hiyo toka mwaka 2016, kumekuwa na mivutano kati ya vyama vya upinzani na vyombo vya usalama ambapo vyombo vya usalama likiwemo Jeshi la Polisi, limekuwa likizuia mikutano kadhaa ya kisiasa kwa madai ya taarifa za kiintelijensia kuonyesha kuna viashiria vya uvunjifu wa amani.

Zuio hilo liliendelea hata alipoingia madarakani, Rais Samia Suluhu kuchukua nafasi ya Magufuli aliyefariki mwezi Machi 2021. Alipozungumza na wahiri wa vyombo vya habari mwezi Juni, Rais Samia aliomba apewe muda kwanza ajenge uchumi wa nchi hiyo, kabla ya kuangalie masuala ya siasa na katiba mpya.

'Nipeni muda tuimarishe uchumi kwanza kisha tuyashughulikie mambo ya katiba na mengine ya siasa'-Rais Samia Suluhu.

Hata hivyo mwishoni mwa wiki hii Msemaji wa Serikali, Gerson Msigwa akizungumza na wanahabari jijini Mwanza, alisema hakuna chama cha siasa kilichozuiwa kufanya mikutano ya siasa, suala ni utaratibu.

'Hakuna mkutano wa mwanasiasa uliozuiliwa. Kilichopo ni utaratibu na si mkutano tu ukienda kufanya shughuli yoyote ambayo vyombo vya ulinzi na usalama vinaona zinahatarisha usalama na vyenyewe vina wajibu kwa mujibu wa sheria kuzuia shughuli hiyo, sio lazima uwe mkutano hata sherehe ya kuzaliwa kama ina viashiria vya uvunjifu wa usalama' - alisema Msigwa.

Katibu mkuu wa chama cha ACT Wazalendo, Addo Shaibu alitofautina na Msemaji huyo wa Serikali akisema haiwezekani mikutano yote ya upinzani ikawa na viashiria vya uvunjifu wa amani.

'Si kweli kwamba mikutano yetu imekuwa na viashiria vya uvunjifu wa amani, tumekuwa tukifanya mikutano hiyo tangu mifumo ya mageuzi ya vyama vingi ubishe hodi Tanzania katika miaka ya 1990s mpaka mpaka mwaka 2016, nini ambacho kiliwezekana kwa miongo miwili ya vyama vingi,kinashindikana kuanzia 2016', alihoji Shaibu alipohojiwa na BBC, kama moja ya vyama vinavyolalamika kuzuiwa kufanya mikutano ya hadhara.

aaa

CHANZO CHA PICHA,EATV

Maelezo ya picha,

Addo Shaibu, Katibu mkuu wa chama cha ACT- Wazalendo

Mbali na mikutano ya siasa, kumekuwa na malalamiko hasa kutoka vyama vya upinzani, vinavyozuiwa hata kukusanyika kwenye shughuli za kawaida ikiwemo kufanya mazoezi ya pamoja(jogging).

Akizungumzia hilo Msigwa alisisitiza kinachofanyika kinafanyika kisheria; 'kama walizuia kwenye kukimbia, sijui kwenye nini, mimi sijui hayo yalikuwaje, lakini hayo ni mamlaka ya kisheria ya vyombo vyetu vya ulinzi na usalama',

Upinzani unasemaje kuhusu kusimamishwa kwa maandamano na mikutano hasa ya hadhara ya kisiasa?

Viongozi wengi wa vyama vya upinzani malalaimiko yao makubwa yapo kwneye kuzuiwa kwa mikutano na shughuli zingine zinazohusisha wafuasi wao kwenye kujenga vyama vyao.

Kwa mujibu wa sheria, vyama vya siasa vinaruhusiwa kufanya mikutano yao ya hadhara ya ndani na nje, huku maandamano yakiruhusiwa pia na sheria za nchi hiyo. Lakini ipo sheria inayotoa wajibu kwa vyombo vya ulinzi na usalama vinapoona kuna viasheria vya uvunjifu wa amani kuzuia mikutano na maandamano.

' Hapa ndipo mgogoro wa tafsiri ya sheria hizi, unapoanzia, pengine kila upande una hoja, lakini wapi wanakutana kukubaliana hoja hizi, hapa ndipo umuhimu wa mkutano huu wa wadau wa siasa Dodoma unapokuja', alisema Beatrice Kimaro, mchambuzi wa siasa Tanzania.

Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe ambaye anashikiliwa kwa tuhuma ugaidi aliwahi kusema mwanzoni mwa mwaka jana kabla ya kukamatwa kwake kwamba kuzuiwa kwa mikutano ya hadhara kumeviathiri vyama vingi vya upinzani na kwamba baadhi ni kama vimekufa.

Chama cha NCCR Mageuzi, chenyewe kilimtaka Rais Samia, kutafakari upya pamoja na mambo mengine kuhusu suala mikutano ya hadhara, kwa kuwa ni suala la kisheria liruhusiwe.

Mkutano huu kumaliza unaodaiwa kuwa 'mzozo' wa siasa Tanzania?

sd

CHANZO CHA PICHA,GETTY IMAGES

Maelezo ya picha,

Rais Samia

Aprili 22 mwaka huu, akitoa hotuba yake ya kwanza iliyotoa dira ya serikali yake ndani ya Bunge jijini Dodoma, Rais Samia alieleza azma yake ya kutaka kuonana na vyama vya kisiasa nchini.

Kikao hicho kilitegemewa na wengi kufanyika mara moja tu baada ya tamko hilo. Ila mambo yamekwenda kando ya matarajio ya wengi. Hadi sasa bado hakijafanyika.

Alipoulizwa kuhusu ahadi hiyo na BBC, Rais Samia alieleza bado ana nia ya kukutana na viongozi wa upinzani. Ingawa hakuweka wazi siku rasmi ya kukutana nao.

Pengine mkutano huu, ni hatua muhimu ya dhamira ya Rais Samia ya kujadiliana na vyama vya siasa na wadau wengine wa siasa, ili kupata hatma ya siasa za nchi hiyo na namna zinavyoweza kufanyika, bila kubughudhi shughuli zingine za ujenzi wa nchi na uchumi wake.

Wengi wanauliza mkutano huu utakuwa mwarobaini wa siasa za Tanzania?

'ukiniuliza mie, ni hatua muhimu na ya kupongeza kuelekea huko, lakini inahitajika zaidi kuzitazama sheria na usimamizi wake, huu ndio msingi wa majadiliano ya mkutano huo, wakikubaliana kwa misingi ya kisheria, utamaduni na utaratibu utatumika kwa misingi hiyo', alisema Kimaro, ambaye ni mhadhiri wa chuo kikuu cha Ushirika Moshi na kuongeza 'iwe rais anakutana na wadau wa siasa ama waziri mkuu, la msingi ni dhamira ya serikaloi nzima, kama dhamira hiyo, matunda ya mkutano huu yataonekana wazi'