WATU watano wanaosadikiwa kuwa ni majambazi wameuwawa na Jeshi la Polisi Mkoani Kigoma katika Ziwa Tanganyika baada ya kutekeleza uporaji wa vifaa mbalimbali vya uvuvi.
Kamanda wa Polisi Mkoani Kigoma, ACP James Manyama amesema vitu vilivyokuwa vimeporwa na kupatikana ni pamoja na mashine tatu za boti, simu za wavuvi pamoja na nyavu za kuvulia samaki, tukio ambalo limetokea usiku wa kuamkia leo Jumatatu, Desemba 20.
ACP Manyama anasema watu wawili wamefariki baada ya kujeruhiwa huku wengine watatu wakitokomea katika Ziwa Tanganyika baada ya kupigwa risasi na kujirusha ndani ya maji na juhudi za Jeshi la Polisi kutafuta miili ya waliozama bado zinaendelea.
“Vitendo vya utekekaji kwa njia ya barabara sasa kudhibitiwa lakini sasa majambazi wamejipeleka kwenye maji lakini sisi Jeshi la polisi nchi kavu tupo na majini tupo ni bora sasa watu wakabadili maisha kwa kufanya kazi halali kuliko kushiriki kwenye vitendo vya kiharifu, na hii ni salamu tu kwamba hatulali waache ujambazi,” amesema RPC Manyama.
Baadhi ya wavuvi wamepongeza hatua hiyo iliyochukuliwa na Jeshi la Polisi la kudhibiti uhalifu ambao umekuwa ukifanyika katika Ziwa hilo na watu mbalimbali na kuhatarisha shughuli za Uvuvi katika ziwa Tanganyika.
0 Comments