Watu wanne waliuawa na wengine zaidi ya 30 kujeruhiwa baada ya mashambulizi matatu ya kujitoa mhanga mjini Kampala mwezi Novemba
Mahakama nchini Uganda imewashtaki watu 15 - akiwemo mwanamke mjamzito - kwa ugaidi kwa madai ya kuhusika katika mashambulizi kadhaa nchini humo.
Wengi wa watuhumiwa walishtakiwa kuwa wanachama wa Allied Democratic Forces (ADF), kundi la wanamgambo ambalo ni sehemu ya kundi la Islamic State.
Mamlaka inasema kundi hilo linahusika na milipuko minne ya hivi majuzi.
Uganda ilianzisha operesheni ya kijeshi dhidi ya ADF katika nchi jirani ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo.
Kundi hilo la wapiganaji liliundwa katika miaka ya 1990 na Waganda ambao hawakufurahishwa na jinsi serikali inavyowatendea Waislamu, lakini walitimuliwa na kuondolewa katika kambi katika eneo la magharibi la milima ya Rwenzori, ambako wapiganaji wake walikuwa wakishambulia vijiji na kuchoma shule mapema miaka ya 2000.
Mashambulizi ya mwezi Oktoba na milipuko mitatu ya kujitoa mhanga katika mji mkuu, Kampala, mwezi Novemba yalitisha mamlaka kuhusu mbinu za kundi hilo zinazobadilika.
Polisi wameliambia shirika la habari la AFP kuwa washukiwa hao 15 wanakabiliwa na mashtaka ya ugaidi, kusaidia na kufanikisha vitendo vya ugaidi, na kuwa wanachama wa kundi la kigaidi, na wataendelea kuzuiliwa hadi watakapofikishwa tena mahakamani tarehe 13 Januari.
Washtakiwa hawakujibu mashtka dhidi yao.
Mapema mwezi huu DR Congo iliidhinisha ombi la Uganda la kuanzisha mashambulizi yanayohusisha mashambulizi ya anga na wanajeshi wa nchi kavu katika eneo la mashariki dhidi ya wanamgambo wa ADF.
0 Comments