Vijana waliohitimu vyuo vikuu nchini wametakiwa kuacha kuchagua kazi na kujiingiza kwenye ujasiriamali na kilimo ili kupata kipato kitakachowawezesha kujikwamua kiuchumi.
Rai hiyo imetolewa na Katibu wa Halmashauri Kuu ya Taifa Uchumi na Fedha ya Chama cha Mapinduzi (CCM), DK Frank Hawaas wakati akizungumza kwenye kongamano la elimu la vyuo na vyuo vikuu Mkoa wa Kilimanjaro.
Dk Hawaas ambaye ni mlezi wa vyuo na vyuo vikuu Taifa amesema tatizo la ajira nchini limeondoa mwelekeo wa vijana wengi na kusababisha kupatikana kwa vijana wasio waadilifu hivyo ni wakati wa vijana wasomi kujiingiza kwenye shughuli za ujasiriamali na kuepuka kuchagua kazi.
"Changamoto ya ajira imeondoa mwelekeo wa vijana wengi na kusababisha kupata vijana ambao wamekosa uadilifu, wengine kukata tamaa na kuonekana kama mzigo kwa jamii na kwa familia, niwaombe ondoeni hofu na wakati mnatafuta ajira, msichague kazi, zipo kazi za aina nyingi ambazo zinaweza kuwaingizia kipato".
Ameongeza kuwa "Tafsiri ya kazi wengine tumeitafsiri vibaya, maandiko yameandika kila kazi iliyo halali inafaida, mimi nimevua samaki, mimi ni mkulima na ni mfugaji ni maisha niliyoishi, lakini pia nilipohitimu nilikuwa kibarua wa kufyeka nyasi Chuo Kikuu cha Ushirika Moshi ili nipate fedha, kwa hiyo usichague kazi kama unataka mafanikio".
"Zipo kazi za aina nyingi, zipo za uzalishaji kulingana na mazingira yetu na zile za huduma, lakini zote hizi ukizifanya kwa waledi na uaminifu, huwezi kukosa kufanikiwa, tumia muda wako vizuri ili uweze kufanikisha ndoto na maono yako, weka malengo unataka kuwa nani baada ya mwaka mmoja, miwili na kuendelea ili ujitume zaidi" amesema
Amewataka vijana kuepuka kutumika vibaya kisiasa na watu wenye nia ovu na chama hicho, hasa katika kipindi hiki cha kuelekea uchaguzi wa ndani ya chama.
Mwenyekiti wa CCM Wilaya ya Moshi Vijijini, ambaye ni mlezi wa vyuo na vyuo vikuu Mkoa wa Kilimanjaro, Siril Mushi amesema lengo la kongamano hilo ni kupokea wanachama wapya na kuwafundisha vijana mbinu za kujiajiri na kujiongezea kipato.
"Niwasihi vijana muwe wajasiri, kwani wengi mnaogopa kwenda sekta binafsi kwa kuogopa kushindwa, tunawapa mbinu za kujiajiri wenyewe kwa kuanza na ajira ndogondogo na katika ujasiriamali ni lazima mtambue mlipo na malengo yenu ni nini, lakini pia muwe na uvumilivu, msiogope ushindani" amesema Mushi
Mwenyekiti wa umoja wa Vijana wa Chama cha Mapinduzi (UVCCM) Mkoa wa Kilimanjaro, Ivan Moshi amesema ajira imekuwa ni tatizo kubwa kwa vijana na kuomba chama na Serikali kuibua fursa mbalimbali za ajira ili kuwezesha vijana wengi zaidi kupata ajira.
0 Comments