RAIS wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe.Samia Suluhu Hassan akielekea katika ukumbi wa mkutano wa Hoteli ya Golden Tulip, Uwanja wa Ndege kwa ajili ya Uzinduzi wa Nembo ya Tarehe ya Sensa ya Watu na Makazi ya Mwaka 2022, (kulia kwa Rais) Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe.Dk.Hussein Ali Mwinyi na Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe.Dkt,.Philip Isdor Mpango..


Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan ameagiza viongozi kutoa elimu na mafunzo kwa wananchi wote ili wajitokeze na kushiriki katika Sensa ya Watu na Makazi inayotarajiwa kufanyika tarehe 23 Agosti, 2022.

Rais Samia ametoa agizo hilo leo wakati akizindua Nembo na tarehe ya Sensa ya Watu na Makazi ya mwaka 2022 katika Hoteli ya Golden Tulip.

Aidha, Rais Samia ameeleza kuwa ili Sensa ifanikiwe, uelimishaji na uhamasishaji ni masuala yanayotakiwa kupewa kipaumbele kuwasaidia wananchi kutoa taarifa kwa ajili ya kuiwezesha Serikali kupata takwimu sahihi zitakazoiwezesha kupanga mipango ya maendeleo ya kiuchumi na kijamii.

Rais Samia pia, amesisitiza elimu hiyo kutokana na changamoto za baadhi ya mila, desturi na imani potofu kwa baadhi ya jamii ambazo zinachukulia kuhesabiwa au kutaja idadi ya watoto au wanakaya waliopo ni kukaribisha laana na mkosi.

Vile vile, Rais Samia ameeleza mwenendo wa baadhi ya jamii au familia kuwaficha na kuwazuia watu wenye ulemavu kutoshiriki katika kuhesabiwa ni kinyume na haki za binadamu.

Kwa upande mwingine, Rais Samia ametoa wito kwa taasisi za Serikali na taasisi binafsi kutumia Nembo ya Sensa katika shughuli zote za kiserikali na za sekta binafsi ili kuitangaza Sensa hadi itakapokamilika.

Tangu kuasisiwa kwa Muungano wa Tanzania, tayari zimefanyika Sensa nyingine tano katika miaka ya 1967, 1978, 1988, 2002 na 2012.



ZuhuraYunus