Kukamilika kwa mradi wa maji wa Jet Buza kunamaliza kilio cha muda mrefu cha wakazi wa kata hiyo na maeneo jirani  wakitarajia kuachana na utegemezi wa maji ya visima.

 
Mhandisi Sijapata Athuman wa Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira(Dawasa) ambao ndio watekelezaji wa mradi huo amesema sasa wakazi wa Buza watakuwa na uhakika wa maji safi na salama.


 
Akizungumza katika mkutano na wakazi wa Buza mtaa wa Amani Athuman amesema kiasi cha Sh2,2 bilioni kimetumika kutekeleza mradi huo hivyo wananchi wanapaswa kuutumia kupata matunda yake.
 
"Ni muda muafaka sasa kwa Wananchi kujitokeza kwa wingi waunganishiwe maji, Serikali kupitia Dawasa imewekeza fedha nyingi katika mradi huu ili kuhakikisha inamtua mama ndoo kichwani basi tuitumie fursa hii kuweza kunufaika na mradi huu na kupata huduma," amesema  Athuman.
 
Akizungumza kwenye mkutano huo ofisa huduma kwa wateja Dawasa,  Eva Kessy  amewaeleza wakazi hao kuwa mamlaka hiyo  ipo tayari kuwahudumia muda wote na hivyo wasisite kujitokeza pale wanapopata changamoto yeyote kuhusu huduma ya majisafi.
 
Mwenyekiti wa Mtaa wa Amani, Omar Katoto  amewasisitiza wananchi wa mtaa huo kuitumia fursa ya kupata majisafi kwa mkopo na kuacha kutumia huduma ya maji ya  Visima.
 
"Tunaishukuru Serikali ya awamu ya Sita chini ya Rais Samia Suluhu, awali wananchi wetu walilalamika kuwa gharama za maunganisho ni kubwa lakini sasa tumeambiwa huduma tutaipata kwa mkopo, hii ni fursa ya sisi sote kuungwanishiwa huduma ya maji”amesema Katoto.
 

Hivi karibuni, Ofisa Mtendaji Mkuu wa Dawasa , Mhandisi Cyprian Luhemeja alisema mamlaka imejipanga vyema kuhakikisha kila mkazi wa Dar es Salaam na Pwani anapata huduma ya maji safi bila kikwazo na wananchi watapata maunganisho ya maji kwa mkopo.
 
Mradi wa maji Jet - Buza utanufaisha wakazi 176,000 katika maeneo ya Yombo, Vituka, Buza, Makangarawe, Machimbo, Sigara, Mji mpya, Kivule, Mwanagati, pamoja na mashine namba 5 ya maji.