Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Nape Nnauye amewataka wananchi katika maeneo ilipojengwa minara ya mawasiliano ya simu kupitia Mfuko wa Mawasiliano kwa Wote (UCSAF) kuilinda, kuitunza na kuitumia kwa kuwa uwekezaji huo mkubwa umeigharimu Serikali fedha nyingi.

Waziri Nape alisema hayo mjini Morogoro wakati akizindua kikao cha Baraza la Wafanyakazi la Mfuko wa Mawasiliano kwa Wote, Juni 28, 2022.

Alisema, Serikali imetumia fedha nyingi kujenga minara hiyo, hivyo ni wajibu kwa wananchi katika maeneo ilipo kuilinda na kuitunza minara hiyo  ili kuiwezesha Tanzania ya kidigitali.

Waziri Nape alisema mnara mmoja wa mawasiliano ya simu kwa kiwango cha chini gharama zake ni zaidi ya Sh300 milioni ni  uwekezaji mkubwa umefanyika, hivyo kushindwa kuilinda, kuitunza  na kutoitumia jambo hilo siyo sawa.

“Nikiwa Waziri napenda kutoa wito kwa Watanzania kuhakikisha wanakuwa walinzi na kuitumia kwa sababu kuiweka isitumike ni hasara wananchi wajitahidi muitumie kwani dunia ya leo taarifa zipo mikonini kwako, ukiwa na Access  (matumizi kwa njia ya kidigitali), mnara umejengwa , tuitumie na tuone namna tutakavyosonga mbele,”alisema Nape.Aidha Waziri Nape amesema katika hotuba ya Bajeti na mpango wa bajeti kwa mwaka 2022/2023, Wizara imebainisha  minara itakayojengwa kwa mwaka huu katika maeneo mapya  ni zaidi ya 700.

Waziri amesema msingi mkubwa katika bajeti hiyo imezungumzia kuwa Tanzania ya kidigitali na haitaweza  kufikiwa bila  ya mawasiliano ya uhakika  na kuisambaza maeneo yote nchini.

Waziri Nape amesema kwa sehemu kubwa minara iliyojengwa inafanya kazi vizuri kutokana na kuwepo kwa makubaliano kati ya UCSAF na Shirika la Umeme la Tanesco  kufungiwa umeme na mingine umeme wa jua (Sola) na majenereta yakiwa yamewekwa kwa tahadhali pekee.

Kuhusu mahusiano mahala pa kazi, Waziri Nape amewataka viongozi wa Taasisi zilizopo chini ya Wizara  yake ukiwemo Mfuko wa Mawasiliano kwa Wote na kwamba  Mabaraza ya Wafanyakazi yatumike namna ya kujadiliana namna bora ya watu kupata haki zao kwa wakati  na hilo ni suala la msingi.


Naye Mwenyekiti wa Bodi ya Mfuko wa Mawasiliano kwa Wote, Profesa John  Nkoma alisema, baraza hilo limeundwa kwa mujibu wa matakwa  ya kisheria, ni chombo muhimu cha kushauriana sehemu ya kazi.


Pia, Profesa Nkoma amesema, Mfuko wa Mawasiliano kwa Wote utaendelea kuchukua hatua mbalimbali za kuboresha huduma za mawasiliano nchini hasa maeneo ya vijijini.


Kwa upande wake Mtendaji Mkuu wa UCSAF, Justina Mashiba  ambaye ni Mwenyekiti  wa Baraza hilo amesema, mfuko  umejipanga kuhakikisha kuwa Watanzania wanaishi vijijini wanapata huduma bora za mawasiliano bila vikwazo .