Washambuliaji ambao walizuiliwa katika eneo la Bryansk mapema leo asubuhi "walikuwa na nia ya kuvuka hadi Ukraine" na walikuwa na "mawasiliano kwa upande wa Ukraine", shirika la usalama la Urusi limesema, kulingana na shirika la habari linalomilikiwa na serikali ya Urusi Ria Novosti.

Ilitarajiwa sana kwamba Urusi ingejaribu kuihusisha Ukraine na mashambulizi hayo, na madai ya FSB katika hatua hii hayawezi kuthibitishwa kwa uhuru.

Wakati habari za shambulio hilo zilipoibuka jana usiku, Mykhailo Podolyak, mshauri wa Rais wa Ukraine Volodymyr Zelensky, alikanusha kabisa kuhusika kwa Ukraine, akisema nchi yake "haina uhusiano wowote na matukio haya".

Urusi ilianzisha uvamizi wake nchini Ukraine mnamo Februari 2022 na imekuwa kwenye vita na jirani yake tangu wakati huo.