Duru za usalama nchini Iraq zinasema kuwa mlipuko mkubwa umepiga kambi ya kijeshi ambayo ina wanamgambo wanaoiunga mkono Iran.

Mjumbe wa kundi la Popular Mobilization Forces ameuawa na wengine wanane kujeruhiwa katika mlipuko huo. Makao makuu ya ulinzi ya Marekani Pentagon yaliharakisha kusema kwamba hawakuhusika katika tukio hilo.

Hakuna mtu mwingine aliyesema pentagon ilihusika kwa sasa, na vyanzo vya usalama nchini Iraq bado havijasema ni nani wanaamini kuwa huenda alipanga shambulio hilo.

Hii inakuja wakati kukiwa na tahadhari kubwa katika Mashariki ya Kati, wakati makabiliano ya muda mrefu kati ya Israel na Iran yameingia katika awamu mpya.

Siku ya Ijumaa, shambulio linalodhaniwa kuwa la Israel lilifanyika karibu na mji wa Isfahan nchini Iran - katika jibu dhahiri la shambulio kubwa la ndege isiyo na rubani na kombora ambalo Tehran ililitekeleza dhidi ya Israeli siku sita zilizopita.

Shambulio hilo pia lilikuwa ni kulipiza kisasi kwa shambulio la awali dhidi ya makamanda wakuu wa jeshi la Iran huko Damascus.

Mzozo huo bado unaonekana kuzuiliwa kwa kiasi fulani kwa sasa, lakini waziri wa mambo ya nje wa Iran ameonya kuwa Iran itatoa jibu la juu zaidi ikiwa Israel itaanzisha mashambulizi makubwa kwa maslahi yake.