Kariakoo ni soko kubwa zaidi la kibiashara nchini Tanzania

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan, ametoa maelekezo kwa Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa, kuongeza saa 24 za uokoaji katika jengo lililoporomoka Kariakoo.

“Waziri Mkuu, ninatambua utaratibu wa uokoaji una muda maalumu wa saa 72 mpaka kusitisha zoezi hilo. Binafsi nina matumaini Mungu anaweza akatenda miujiza na kuwanusuru ambao bado wamenaswa. Ninakupa maelekezo kutositisha zoezi la uokoaji na kuongeza muda wa saa 24 zaidi,” amesema Rais Samia kwa njia ya simu.

Vifo vya watu 16 vimethibitishwa tangu kuporomoka kwa jengo la ghorofa Novemba 16, 2024 katika soko kubwa la kibiashara la Kariakoo, katika mkoa wa Dar es Salaam

Juhudi za uokoaji zinazoongozwa na vikosi mbali mbali vya serikali na taasisi binafsi, zinaendelea huku serikali ikitangaza kuwa zaidi ya watu 80 wameokolewa kufikia siku ya jana.