Ukraine imesema haitakubali kamwe uchokozi wa Urusi kwani inaadhimisha siku 1,000 tangu Kremlin ianzishe uvamizi dhidi ya nchi hiyo.

"Ukraine haitasalimu amri kwa wavamizi, na jeshi la Urusi litaadhibiwa kwa kukiuka sheria za kimataifa," wizara ya mambo ya nje ilisema Jumanne.

Zelensky baadaye atahutubia kikao maalumu cha Bunge la Ulaya wakati nchi hiyo ikiadhimisha hatua hiyo muhimu.

Hatua hiyo inakuja wakati watu wanane, akiwemo mtoto, waliuawa katika shambulio la ndege isiyo na rubani kwenye eneo la kaskazini-mashariki mwa Ukraine la Sumy usiku kucha, ambapo watu 89 pia waliuawa katika shambulio tofauti siku ya Jumapili.

Shambulio la ndege zisizo na rubani kwenye jengo la makazi katika mji mdogo wa Hlukhiv limejeruhi watu 12 wakiwemo watoto wawili, jeshi la polisi la taifa la Ukraine lilisema.

Rais Zelensky aliandika kwenye X kwamba jengo hilo lilikuwa bweni katika shule ya mtaani.

"Urusi inaendelea kutisha mikoa yetu ya mpaka," Zelensky aliandika. Katika video iliyosambazwa na rais, wafanyakazi wa dharura walionekana wakipekua vifusi walipokuwa wakiendelea kutafuta waathiriwa Jumanne asubuhi.

Zelensky alisema shambulio hilo lilithibitisha kwamba Putin "anataka vita viendelee, hana nia ya kuzungumza juu ya amani".