MAMLAKA ya Uhifadhi na Uendeshaji wa Mji Mkongwe Zanzibar kwa kushirikiana na taasisi nyingine za serikali zimewaruhusu vijana wapiga makachu katika eneo la Forodhani kuendelea na shughuli zao kwa kuzingatia taratibu zilizoanishwa katika mikataba watakayosaini.
Mkurugenzi Mkuu wa mamlaka hiyo, Ali Said Bakari amesema hayo ikiwa ni takribani juma moja limepita tangu vijana hao kukatazwa kupiga makachu katika eneo la Forodhani baada ya kukiukwa taratibu ikiwemo suala la maadili na uharibifu wa mali za serikali.
Alisema shughuli za makachu zitaendelea kwa vijana watakaokua tayari kusaini mkataba na kuridhia masharti yaliyowekwa ili kufanya shughuli hizo bila kuvunja sheria na taratibu za nchi.
Shughuli za upigaji makachu zimeruhusiwa tangu Desemba 31, 2024 ikiwa ni sehemu pia ya kuukaribisha Mwaka Mpya 2025 ambapo shughuli hizo zimekuwa ni sehemu kubwa ya ajira kwa vijana ambao waliathirika na katazo hilo kwa takribani wiki moja.
0 Comments