MOROGORO: CHUO Kikuu Sokoine cha Kilimo (SUA) kimepata miradi tisa ya utafiti katika nyanja mbalimbali yenye kugharimu zaidi ya Sh bilioni 3.8 kwa kipindi cha Oktoba 2024/2025.

Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu hicho, Profesa Raphael Chibunda amesema hayo mbele ya mkuu wa chuo hicho na Waziri Mkuu Mstaafu, Jaji  Mstaafu Joseph Warioba wakati wa mahafali ya 45 yaliyofanyika Kampasi ya Edward Moringe, Mjini Morogoro.

Profesa Chibunda amesema licha ya kupata miradi hiyo ya utafiti, SUA inaendelea na utekelezaji wa Mradi wa Elimu ya Juu kwa Mageuzi ya Kiuchumi (HEET) ambapo kimesaini mikataba ya ujenzi na ukarabati wa majengo mbalimbali yenye jumla ya thamani ya Sh bilioni 58.5.

“Wakandarasi kwa ajili ya utekelezaji wa miradi hiyo wanaendelea na kazi zao, “ amesema Profesa Chibunda.

Mbali na utekelezaji wa miradi hiyo ya HEET, Profesa Chibunda amesema mwezi Februari mwaka huu chuo kilizindua kigoda cha utafiti cha Shirika la Maendeleo la Kimataifa la Japani (JICA).

SOMA ZAIDI: SUA yaeleza mafanikio miaka mitatu ya Samia – HabariLeo

Kigoda hicho ni kwa ajili ya kuboresha kilimo cha umwagiliaji na kituo cha teknolojia kwa ajili ya kuhamasisha utekelezaji wa kilimo na viwanda kwa kutoa mafunzo pamoja na ushauri kwa wajasiriamali wadogo na wakati  na uchakataji wa mazao.

Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu hicho ametaja eneo lingine ni utengenezaji wa bidhaa za misitu na kuboresha bidhaa za wakulima na wasindikaji wadogo.

“Chuo kinawashukuru wadau mbalimbali kwa misaada yao mbalimbali iliyochangia kukifikisha chuo kilipo ikiwa na shukrani kwa Rais Dk Samia Suluhu Hassan kwa serikali yake kuendelea kulipia gharama za uendeshaji wa chuo chetu.” amesema Profesa Chibunda.

Kwa upande wa mahafali hayo amesema jumla ya wahitimu 794 kutoka Programu 77 za masomo,  wametunukiwa shahada za kuhitimu elimu ya Chuo Kikuu,  kati ya hao wanaume ni 495 na wanawake 299.

“Idadi ya wanawake waliohitimu katika mahafali haya ni sawa na asilimia 37.7 ya wahitimu wote” alisema Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu hicho” amesema Profesa Chibunda.

Profesa Chibunda amesema wahitimu wa Shahada za Kwanza ni 677, Shahada za Umahiri 80 ambapo wanaume ni 53 na wanawake 27, Shahada ya Uzamivu 25 kati yao  wanaume 17 na wanawake wanane ,huku wahitimu wa Stashahada  ni wanane (na wahitimu wa Astashahada ni wanne .

‘‘Tunastahili kujipongeza kwa mafanikio tunayoendelea kuyapata kila mwaka ya kuongeza idadi ya nguvu kazi katika Taifa,” amesema Profesa Chibunda.

“…Viongozi wa Chuo, wanataaluma na wafanyakazi wote wanastahili pongezi kwa kufanya kazi nzuri inayowawezesha kupiga hatua zaidi za mafanikio chuoni mwaka hadi mwaka, ukizingatia kuwa kuhitimu katika Chuo hiki haijawahi kuwa lelemama,” amesisitiza  Profesa Chibunda.

Kwa upande wake Makamu Mwenyekiti wa Baraza la Chuo Kikuu hicho,Dorothy Mwanyika, ambaye alimwakilisha  Mwenyekiti wa Baraza la Chuo, Andrew Massawe, amesema katika kipindi cha kutoka Mahafali ya 44  ya  Oktoba 2024 mambo mengi yamefanyika na Baraza la Chuo limeendelea kusimamia shughuli za chuo na kupitisha maamuzi mbalimbali ili kuboresha utendaji na ufanisi wa maendeleo ya chuo.