Shujaa wa ngumi za uzito wa juu duniani raia wa Uingereza, Anthony Joshua, amejeruhiwa katika ajali ya gari iliyotokea leo katika barabara kuu ya Ogun–Lagos, Nigeria, ambapo watu wawili wamefariki dunia.

Polisi wa jimbo la Ogun wamesema kuwa Joshua, mwenye umri wa miaka 36 na mzaliwa wa familia yenye asili ya Sagamu, Nigeria amepata majeraha madogo lakini yupo salama. Wengine waliokuwa wamejeruhiwa walikimbizwa hospitalini..

Vyombo vya habari vya ndani vimeripoti kuwa Joshua alikuwa nyuma ya dereva wakati gari lake, aina ya Lexus, lilipogonga lori lililokuwa limeegeshwa. Mashuhuda walisema kuwa gari hilo lilikuwa na abiria wanne, akiwemo Joshua. Watu wake wa ulinzi walikuwa katika gari lingine lililokuwa nyuma yao kabla ya kutokea kwa ajali hiyo.

Masaa machache kabla ya ajali, Joshua alishiriki video kwenye Instagram akiwa akicheza tenisi na mtu mwingine. Joshua alikuwa nchini Nigeria baada ya mechi yake na Jake Paul mnamo 19 Desemba, lakini haijajulikana kwa uhakika wakati na mahali video hiyo ilipigwa.

Polisi na vyombo vya habari vya ndani vinaendelea kufuatilia hali ya Joshua na pamoja na uchunguzi zaidi wa ajali hiyo.