Ghana imewatimua raia watatu wa Israel waliowasili nchini humo siku ya Jumatano katika kile kinachoonekana kuwa ni kitendo cha kulipiza kisasi kutokana na madai ya Israel kuwatendea vibaya raia wa Ghana katika uwanja wa ndege wa kimataifa wa Ben Gurion nchini Israel.
Raia saba wa Ghana, wakiwemo wajumbe wanne wa ujumbe maalumu waliokuwa wakihudhuria mkutano wa usalama wa mtandao huko Tel Aviv, walizuiliwa.
Waliachiliwa baada ya saa tano, huku wengine watatu wakifukuzwa, kulingana na Ghana, ambayo iliyakosoa "matendo hayo kama yakufedhehesha."
Wizara ya mambo ya nje ya Ghana inasema mwanadiplomasia mkuu kutoka ubalozi wa Israel mjini Accra aliitwa kuhusu tukio hilo, na nchi zote mbili zimekubaliana kutatua mzozo huo kwa amani.
BBC imewasiliana na ubalozi wa Israel kwa maoni lakini bado haijapata jibu.
Chanzo cha mvutano kati ya Ghana na Israel hakiko wazi, lakini msimamo wa hivi karibuni wa Ghana kuhusu mzozo wa Israel na Palestina unaweza kuwa sababu.
Mwezi Septemba, Ghana ililaani mashambulizi ya anga ya Israel yaliyoikumba Qatar, na kuyataja mashambulizi hayo kama "ukiukwaji wa wazi wa sheria za kimataifa" na kudharau mamlaka ya Qatar.
Mwezi uliopita, Ghana iliitaka Israeli kuruhusu misaada zaidi kuingia Gaza, ikielezea mateso ya wakaazi wa Gaza kuwa "ya kuvunja moyo."
Rais John Mahama alitoa tani 40 za chokoleti na bidhaa za kakao zinazotengenezwa Ghana kwa Wapalestina, na kuthibitisha uungaji mkono wa muda mrefu wa nchi hiyo kwa kadhia ya Palestina na suluhisho la mataifa mawili kwa mzozo wa Israel na Palestina.
Wachambuzi wanapendekeza kwamba hatua hizi zinaweza kuwa zimechangia katika hali mbaya ya mahusiano ya sasa, hasa kama Israel inaona msimamo wa Ghana kuwa wa upendeleo au usiopendeza.

0 Comments