Waziri mkuu wa kwanza mwanamke nchini Bangladesh Khaleda Zia amefariki dunia akiwa na umri wa miaka 80 baada ya kuugua kwa muda mrefu.

Zia alikuwa mwanamke wa kwanza kuongoza serikali nchini Bangladesh mwaka 1991 baada ya kukiongoza chama chake kupata ushindi katika uchaguzi wa kwanza wa kidemokrasia nchini humo katika kipindi cha miaka 20.

Madaktari walisema Jumatatu kuwa hali yake ilikuwa "mbaya sana."

Licha ya afya yake mbaya, chama chake kilisema hapo awali kwamba Zia atagombea urais katika uchaguzi mkuu unaotarajiwa kufanyika Februari, uchaguzi wa kwanza tangu mapinduzi yaliyosababisha kuondolewa madarakani kwa mpinzani wake Zia, Sheikh Hasina.

Siasa za Bangladesh kwa miongo kadhaa zilikuwa zikiogozwa na wanawake hao wawili.

"Kiongozi wetu tunayempenda hayupo tena," Chama cha Kizalendo cha Bangladesh (BNP) cha Zia kilitangaza kwenye mtandao wa Facebook siku ya Jumatatu.

Zia alionekana hadharani kwa mara ya kwanza kama mke wa rais wa zamani wa Bangladesh Ziaur Rahman. Lakini baada ya kuuawa kwake katika mapinduzi ya kijeshi ya 1981, Zia aliingia katika siasa na baadaye akapanda cheo na kuiongoza BNP.

Baada ya muhula wa pili mwaka 1996 uliodumu kwa wiki chache tu, Zia alirudi katika wadhifa wa waziri mkuu mwaka 2001, akajiuzulu Oktoba 2006 kabla ya uchaguzi mkuu.

Kazi yake ya kisiasa ilikumbwa na madai ya ufisadi na ushindani wa kisiasa wa muda mrefu na kiongozi wa Awami League, Sheikh Hasina, ambaye aliondolewa kutoka wadhifa wa uwaziri mkuu mwaka jana.

Zia alifungwa jela kwa ufisadi mwaka 2018, chini ya utawala wa Hasina. Zia alikana kutenda makosa na akasema mashtaka hayo yalikuwa ya kisiasa.

Aliachiliwa huru mwaka jana, muda mfupi baada ya maandamano makubwa ya kupinga serikali nchini Bangladesh kumpindua Hasina, na kumlazimisha kukimbilia uhamishoni.

Chama cha BNP kilisema mwezi Novemba kwamba Zia atafanya kampeni kwa ajili ya uchaguzi mkuu ujao.

Chama cha BNP kinatazamia kurejea madarakani, na ikiwa hilo litatokea, mwana wa Zia, Tarique Rahman, anatarajiwa kuwa kiongozi mpya wa nchi hiyo.

Rahman, mwenye umri wa miaka 60, amerejea Bangladesh wiki iliyopita tu baada ya miaka 17 ya kuishi uhamishoni jijini London.

Zia alikuwa hospitalini tangu mwezi uliopita, akipokea matibabu ya figo, ugonjwa wa moyo na nimonia, miongoni mwa magonjwa mengine.