Dkt. Flavian Zeija ameteuliwa kuwa Jaji Mkuu wa Jamhuri ya Uganda, akichukua nafasi ya Jaji Alfonse Owiny-Dollo Chigamoy aliyestaafu.
Bunge la Uganda pia limethibitisha kuwa limekamilisha mchakato wa kumsaili na kumuidhinisha Dkt. Zeija.
Ikulu ya Uganda ilithibitisha katika taarifa ya Alhamisi kuwa, kwa kutumia mamlaka aliyopewa Rais chini ya Kifungu cha 142(1) cha Katiba ya mwaka 1995, na kwa ushauri wa Tume ya Huduma za Mahakama, Rais Yoweri Kaguta Museveni amemteua Mheshimiwa Jaji Flavian Zeija kuwa Jaji Mkuu wa Uganda.
Taarifa hiyo ilieleza kuwa uteuzi huo ulifuatia kuwasilishwa kwa jina la Jaji Zeija bungeni kwa ajili ya kuidhinishwa, ambapo Bunge lilitoa idhini hiyo kwa mujibu wa katiba.
Inaripotiwa kuwa Tume ya Huduma za Mahakama iliwasilisha majina ya Jaji Izama Madrama, Mike Chibita na Flavian Zeija kama wagombea waliokidhi vigezo, na kumpendekeza Rais achague mmoja kati yao.
Uteuzi huu umetangazwa siku chache tu baada ya aliyekuwa Jaji Mkuu, Alfonse Owiny-Dollo Chigamoy, kustaafu rasmi baada ya kutimiza umri wa lazima wa miaka 70.
Owiny-Dollo alimkabidhi rasmi ofisi Jaji Zeija, akieleza kuwa sheria inamtaka Jaji Mkuu anayestaafu kumkabidhi madaraka naibu wake iwapo Jaji Mkuu wa kudumu bado hajateuliwa na Rais.
Katika hali hii, Dkt. Zeija amekuwa Jaji Mkuu kaimu tangu Jumatatu alasiri, alipokabidhiwa ofisi hiyo.
Vyanzo vimeeleza pia kuwa kulifanyika tukio jingine la makabidhiano jana bila uwepo wa vyombo vya habari katika makao makuu ya Mahakama, baada ya makabidhiano ya Jumatatu kufanyika kwa haraka ili kuepuka ukosoaji wa umma kuhusu ucheleweshaji wa mchakato huo.
Uteuzi wa Dkt. Zeija umewashangaza wengi ndani ya Mahakama na hata Tume ya Huduma za Mahakama, kwani amepanda cheo kwa kasi kubwa.
Amekaa chini ya mwaka mmoja tu katika nafasi ya Naibu Jaji Mkuu kabla ya kuteuliwa kuwa Jaji Mkuu.
Dkt. Zeija aliteuliwa kuwa Naibu Jaji Mkuu tarehe 7 Februari 2025, akimrithi aliyekuwa Naibu Jaji Mkuu mstaafu, Jaji Richard Buteera. Kabla ya hapo, alikuwa Jaji Mkuu wa Mahakama (Principal Judge), nafasi ambayo baadaye ilishikiliwa kwa kaimu na Jaji Jane Okuo Kajuga kwa takriban mwaka mmoja.
Mwezi uliopita, Rais Museveni alimteua rasmi Jaji Jane Okuo Kajuga, aliyekuwa Naibu Mkurugenzi wa Mashtaka ya Umma, kuwa Jaji Mkuu wa Mahakama (Principal Judge).
Aidha, Spika wa Bunge la Uganda amethibitisha kuwa Jaji Flavian Zeija alisailiwa na Kamati ya Uteuzi ya Bunge baada ya kuteuliwa na Rais Museveni kuwa Jaji Mkuu.
Spika alisema: “Mapema leo, Kamati ya Uteuzi ilikutana na kumsaili Jaji Flavian Zeija, ambaye aliteuliwa na Rais Museveni.”

0 Comments