
TAASISI ya Wanasayansi Wahandisi Wasio na Mipaka (SEWB) ya Korea Kusini imefadhili ujenzi wa mtambo wa kuzalisha gesi asilia ya kupikia ya bayogesi katika Chuo cha Ufundi Stadi cha Wilaya ya Monduli mkoani Arusha kwa gharama ya Sh milioni 124.
Uzinduzi wa mtambo huo ulifanyika mwishoni mwa wiki na Mkurugenzi Msaidizi, Elimu ya Ufundi na Mafunzo ya Ufundi Stadi, Dk Erick Mgaya kwa niaba ya Katibu Mkuu, Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia, Profesa Carolyne Nombo. Profesa Nombo kupitia hotuba yake iliyosomwa na Dk Mgaya amesema mradi huo ni sehemu ya juhudi za serikali katika kufanikisha matumizi ya nishati safi na endelevu ya kupikia nchini.
Amesema ufadhili wa mradi huo kutoka SEWB ni mfano wa ushirikiano kati ya mataifa na taasisi katika kuleta mabadiliko chanya katika jamii. “Teknolojia hii ya bayogesi inapunguza matumizi ya kuni na mkaa kwa kuwa mtambo utatumia taka za kaboni na mabaki ya chakula kuzalisha nishati safi ya kupikia pamoja na matumizi mengine chuoni hapa,” alisema Profesa Nombo.
Ameongeza kuwa teknolojia hiyo inasaidia kulinda misitu na mazingira, kupunguza gharama za nishati kwa taasisi na kuwapa wanafunzi mafunzo ya vitendo katika teknolojia za nishati jadidifu. Mradi huo unaifanya Mamlaka ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi Stadi (VETA) kuwa sehemu ya suluhisho la kimataifa katika kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi na kuchochea maendeleo endelevu.

Mkuu wa Chuo cha Veta Monduli, Theophan Pantaley amesema mradi huo umefadhiliwa na SEWB kwa gharama ya Dola za Marekani 49,700 sawa na Sh milioni 124.3. Amesema mtambo huo una uwezo wa kuzalisha meta za ujazo 100 za bayogesi kwa siku, kiasi kinachoweza kuhudumia wanafunzi 600.
Mkurugenzi wa SEWB, Profesa Minsoo Maeng amesema shughuli za taasisi hiyo zinaendana na sera ya nishati safi ya Tanzania inayolenga kupanua upatikanaji wa nishati salama, nafuu na endelevu ya kupikia. Amesema Serikali ya Jamhuri ya Korea na Serikali ya Tanzania zimeendelea kudumisha ushirikiano katika sekta za elimu, sayansi, teknolojia na maendeleo endelevu.
Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa Veta, Eniart Mahundi amesema mradi huo ni wa pili kufanyika ndani ya Veta kwa ufadhili wa SEWB. Amesema mradi wa kwanza ulitekelezwa katika Chuo cha Ufundi Stadi Arusha (Oljoro) kwa gharama ya Sh milioni 156.8. Mkurugenzi wa VETA Kanda ya Kaskazini, Monica Mbele aliutaka uongozi wa chuo na wanafunzi kuutunza mradi huo ambao ni rasilimali ya umma ili udumu kwa muda mrefu.
Ujenzi wa mtambo huo ulifanywa na Kampuni ya Kitanzania ya ENVSOL Technology Agosti mwaka jana na umekamilika Januari mwaka huu. SOMA: REA yatoa majiko ya gesi 310 kwa maafisa magereza Geita
0 Comments