Jeshi la Iran IRGC limeapa kumfuatilia na kumuua waziri mkuu wa Israel, Benjamin Netanyahu, kwa mujibu wa ripoti za vyombo vya habari vya serikali.

Shirika la habari la Iran, Mehr News Agency, linaripoti kuwa IRGC litaendelea “kumfuatilia na kumuua”.

Aidha jeshi hilo pia linadai kuwa limeharibu maeneo kadhaa ndani ya Israel pamoja na vituo vitatu vya kijeshi vya Marekani katika eneo hilo wakati wa wimbi lake la 52 la mashambulizi.

Wakati huo huo, watu 20 wamekamatwa katika mji wa Urmia nchini Iran wakituhumiwa kutuma taarifa za maeneo ya kijeshi, polisi na usalama kwa Israel.

Kwa mujibu wa Tasnim News Agency, shirika la habari lenye uhusiano na IRGC, mitandao kadhaa ya watu wanaodaiwa kuwa mamluki wanaohusishwa na maafisa wa Israel imefungiwa.

Watu hao 20 walikamatwa kufuatia amri ya mahakama, kwa mujibu wa mwendesha mashtaka mkuu wa jimbo la West Azerbaijan.