Wizara ya Afya ya Lebanon inasema kuwa watu 14 wakiwemo watoto wawili waliuawa Jumapili katika mashambulizi ya Israel.
Msemaji wa Jeshi la Ulinzi la Israel (IDF) hapo awali alitoa ilani ya kuhama kwa wakaazi kutoka vijiji kadhaa kusini mwa Lebanon, na kuonya kuwa wa kupuuza ilani hiyo "kungelihatarisha maisha yao".
IDF baadaye ilisema ilifanya "mashambulizi ya angani" kuwalenga wanamgambo wa Hezbollah katika maeneo ya kusini mwa Lebanon ambayo inadai yanatumiwa "kuendeleza mashambulizi dhidi ya wanajeshiwa Israel".
Pia imesema mwanajeshi wa IDF mwenye umri wa miaka 19 ameuawa na wengine sita kujeruhiwa na shambulio la ndege isiyo na rubani ya Hezbollah nchini Lebanon.
Hezbollah ilirusha ndege tatu zisizo na rubani kuelekea Israeli, IDF iliripoti, huku ikiongeza kuwa ziliangushwa na jeshi la anga la Israeli kabla ya kuvuka mpaka.
Nchi hizo mbili zilifikia mpango wa usitishaji mapigano, ambao ulianza kutekelezwa tarehe 16 Aprili na kuongezwa muda kwa wiki tatu Alhamisi wiki iliyopita.
Chini ya makubaliano hayo, Israel inasalia na "haki yake ya kuchukua hatua zote za kujilinda, wakati wowote, dhidi ya mashambulizi yaliyopangwa, yanayokaribia, au yanayoendelea".
Akizungumza katika mkutano wa serikali, Waziri Mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu alisema IDF "inaendelea, na inafanya kazi kwa nguvu" nchini Lebanon, akisema hatua za Hezbollah "zinasambaratisha usitishaji mapigano"

0 Comments