Marekani, Uingereza na Australia zinasema zitatengeneza teknolojia ya ndege zisizo na rubani chini ya maji ili kulinda nyaya za chini ya bahari na kuongeza ulinzi, chini ya muungano wao wa kijeshi unaojulikana kama Aukus.

Teknolojia hii inatarajiwa kuwa tayari ifikapo mwaka ujao. Ingawa gharama ya jumla ya mradi huo haikutajwa, waziri wa ulinzi wa Uingereza John Healey alisema Uingereza itachangia pauni milioni 150 ($201m).

Tangazo hilo, lililotolewa na mawaziri wa ulinzi wa nchi hizo katika mkutano wa usalama huko Singapore, linafuatia madai ya maendeleo ya polepole katika miradi ya Aukus.

Akikubali ukosoaji huo, Healey alisema "kwa muda mrefu sana huko Aukus, tulizungumza sana na kutenda machache sana", akiongeza "hilo sasa limebadilika chini ya serikali zetu tatu".

Mkataba wa ulinzi wa Aukus, ulioanza mwaka wa 2021, unaziona nchi hizo tatu zikiendeleza manowari za nyuklia na kushiriki utaalamu wa kijeshi.

Hatua hii inaonekana sana kama njia ya kukabiliana na China ambayo imeongeza shughuli zake katika eneo la Indo-Pacific na jukumu lake katika kuongezeka kwa mvutano katika maeneo yenye migogoro kama vile Bahari ya Kusini ya China.