Mkoa wa Mtwara umeendelea kujidhihirisha kama kitovu muhimu cha uwekezaji wa madini nchini kutokana na uwepo wa rasilimali nyingi za madini ya viwandani, vito na madini mkakati, huku mapato ya Serikali kupitia sekta hiyo yakiongezeka kwa kasi katika kipindi cha miaka mitatu iliyopita.

Afisa Madini Mkazi wa Mkoa wa Mtwara, Winnifrida Mrema, amesema mkoa huo unafahamika zaidi kwa uwepo wa madini ya chokaa yanayotumika kuzalisha saruji katika Kiwanda cha Saruji cha Dangote, jambo linalochangia kukuza uchumi wa mkoa na kuimarisha shughuli za viwanda nchini.

Amesema Mkoa wa Mtwara pia una utajiri wa madini mengine ya viwandani yakiwemo chuma, shaba, kinywe, ulanga pamoja na madini ya mchanga mzito (heavy mineral sands), ambayo ni miongoni mwa madini mkakati yanayohitajika kwa kiwango kikubwa duniani katika utengenezaji wa teknolojia mbalimbali ikiwemo magari ya umeme.

Aidha, amesema Bandari ya Mtwara imeendelea kuwa kiungo muhimu cha biashara na usafirishaji wa madini na bidhaa za viwandani, ambapo hutumika kusafirisha saruji ya Dangote kwenda Zanzibar na Visiwa vya Comoro, sambamba na usafirishaji wa makaa ya mawe kutoka mikoa ya Ruvuma na Njombe kuelekea masoko ya China, India na Dubai.

Kwa upande wa uwekezaji, Mrema amesema Mkoa wa Mtwara una fursa kubwa katika uchimbaji na uchakataji wa madini ya dhahabu, shaba pamoja na vito, hususan green garnet, huku akiwahimiza wawekezaji wa ndani na nje ya nchi kutumia fursa hizo kuwekeza katika sekta ya madini.

Pia amesema Serikali inaendelea kuwahamasisha wawekezaji kushirikiana na wachimbaji wadogo wa madini ya viwandani, dhahabu na vito kwa kuwapatia mitaji, mafunzo na msaada wa kitaalam ili kuongeza uzalishaji na kuboresha shughuli zao za uchimbaji.

Akizungumzia mapato ya Serikali, Mrema amesema makusanyo kupitia sekta ya madini mkoani humo yameongezeka kutoka shilingi bilioni 1.85 mwaka 2021/22 hadi shilingi bilioni 5.95 mwaka 2023/24, kabla ya kufikia shilingi bilioni 7.55 mwaka 2024/25, hatua inayoonesha ukuaji mkubwa wa sekta hiyo na mchango wake katika uchumi wa taifa.

Naye Fundi Sanifu Madini kutoka Ofisi ya Afisa Madini Mkazi wa Mkoa wa Mtwara, Nurah Juma, amesema madini ya ujenzi kama mawe na kokoto yanayochimbwa katika kijiji cha Chipite wilayani Masasi yameendelea kuwa mhimili muhimu wa utekelezaji wa miradi ya maendeleo katika mikoa ya Mtwara na Lindi.

Amesema kokoto zinazozalishwa katika eneo hilo zinatumika katika ujenzi wa barabara, majengo, upanuzi wa Bandari ya Mtwara na viwanja vya ndege, pamoja na ujenzi wa Bandari mpya ya Kisiwa Mgao, hali inayochangia upatikanaji wa vifaa vya ujenzi vyenye ubora na kuchochea maendeleo ya kiuchumi katika ukanda wa kusini.