ARUSHA: Tanzania imeendelea kupiga hatua katika sekta ya afya ndani ya nchi za Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC), kutokana na utoaji wa huduma bora za afya katika hospitali mbalimbali nchini.

Aidha, serikali inaendelea kufanyia kazi masuala mbalimbali ya kada ya uuguzi, ikiwemo muundo wa utawala wa Wizara ya Afya pamoja na muundo wa utumishi wa kada hiyo, baada ya madai hayo kuwasilishwa mara kadhaa wizara husika.


Katibu Tawala wa Mkoa wa Arusha, Dk, Toba Nguvila, amezungumza hayo kwa niaba ya Waziri wa Afya, Mohammed Mchengerwa wakati wa ufunguzi wa kongamano la 55 la wauguzi lenye kaulimbiu isemayo, “Wauguzi Wetu, Mustakabali Wetu, wauguzi waliowezeshwa huboresha maisha”, kuelekea maadhimisho ya Siku ya Wauguzi Duniani yanayofanyika Mei 12 .

Amesema Tanzania imepiga hatua hiyo kutokana na juhudi na huduma bora zinazotolewa na wauguzi nchini, huku akieleza kuwa Wizara ya Afya kwa kushirikiana na Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora inaendelea kushughulikia changamoto zinazowakabili wauguzi, na tayari baadhi ya mapendekezo yamefanyiwa kazi.

“Nakubaliana nanyi kuwa uongozi haupaswi kuzingatia taaluma moja pekee, bali uzingatie sifa za kiuongozi, elimu, uzoefu, uadilifu na uzalendo kwani changamoto hiyo msingi wake ni sheria ya afya ya umma pamoja na sera ya afya,nawaelekeza watendaji kuhakikisha mapitio ya mambo haya yanafanyika ili kutoa fursa sawa za uongozi katika sekta ya afya,” amesema.

Amewasihi wauguzi kuendelea kuwa na kauli nzuri, nyuso zenye tabasamu na mioyo ya huruma na upendo kwa wagonjwa, kwani tabia hiyo ni sehemu muhimu ya tiba kwa mgonjwa na familia.

 

Akisoma risala katika kongamano hilo, Katibu wa Chama cha Wauguzi Tanzania, Chacha John, amesema muundo wa utumishi wa kada ya uuguzi na ukunga wa mwaka 2009 hauendani tena na majukumu pamoja na ukuaji wa taaluma hiyo, hali inayosababisha changamoto nyingi ambazo zimekuwa zikiwasilishwa serikalini tangu mwaka 2013.

Ameongeza kuwa licha ya jitihada na mawasiliano ya karibu kati ya chama hicho na Serikali kuhusu utekelezaji wa muundo mpya wa utumishi, bado kwa zaidi ya miaka 13 mapendekezo hayo hayajaanza kutekelezwa.