
KAGERA: Serikali kwa kushirikiana na Benki ya Maendeleo ya kilimo(TADB) inaendelea kutekeleza zoezi la utoaji wa mikopo isiyo na riba na yenye masharti nafuu kwa ajili ya utekelezaji wa miradi ya ufugaji wa samaki kwenye vizimba ili kuwezesha vijana wengi kujiajiri kupitia uvuvi.
Akizungumza katika hafla ya uzinduzi wa kukabidhi mitaji ya kuwezesha utekelezaji wa miradi iliyobuniwa na Vijana wa (Build Better Tomorrow (BBT)-Uvuvi Mkoa wa Kagera katika mwalo wa -Bilolo Kemondo, Mwakilishi wa Katibu Mkuu wa Wizara hiyo, Emelda Adam amesema programu hiyo inalenga kupambana na changamoto ya ajira kwa vijana na kuongeza nguvu ya vijana kujitegemea.

Amesema vijana walionufaika na vizimba mkoani Kagera walipata mafunzo ya ukuzaji wa viumbe hai mwaka 2024 na wametoka mikoa mbalimbali wakiwa wameiva kwa ujuzi wa uendeaji wa vizimba hivyo ambapo wataanza kuvuna Samaki baada ya miezi 7.
Naye, Msimamizi Mkuu wa programu ya “BBT” kanda ya ziwa Peter Masumbuko amesema vijana 47 wa mkoa wa Kagera wamenufaika na programu hiyo ambapo kiasi cha shilingi za kitanzania bilioni 7 zimetengwa kwa ajili ya vijana zaidi ya 300 wa mikoa ya Kanda ya Ziwa.

Awali Mkuu wa Wilaya ya Erasto Sima kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa wa Kagera amesema anamshukuru Rais wa Tanzania Dk Samia Suluhu Hassan kwa ajili ya programu hiyo na kuwaasa vijana wanufaika wa mkopo huo kuutumia kwa malengo yaliyokusudiwa.

Amesema baada ya ufunguzi wa zoezi hilo la vizimba mvuvi yeyote atakayekamatwa katika eneo Hilo arachukuliwa kama mvuvi haramu kwani sehemu hiyo halipaswi kusogelewa badala yake linapaswa kulindwa Kwa nguvu zote ili kuleta matokeo chanya.

Mwenyekiti wa Halmashauri ya Bukoba, Sadothi Ijunga ameishukuru serikali kupitia wizara ya mifugo na uvuvi kwa kuukumbuka mkoa wa Kagera na kuwaasa vijana kuwa na nidhamu katika matumizi ya fedha walizozipata ambapo alisema Halmashauri ya Bukoba Iko tayari kutoa eneo la ujenzi wa chuo cha uvuvi bure.
0 Comments