Akizungumza katika mdahalo huo jana jioni (Jumanne, Mei 26, 2026) katika ukumbi wa kimataifa wa mikutano wa Kintele (Kintele International Conference Centre), jijini Brazzaville, Jamhuri ya Kongo, Waziri Mkuu alisema Tanzania imeendelea kuchukua hatua za kuimarisha sekta binafsi na kuongeza vyanzo vya mapato ya ndani katika kuimarisha uhamasishaji wa rasilimali za ndani.
“Hatua hizo zinaenda sambamba na uamuzi wa Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan wa kuunda tume ya kupitia mifumo ya kodi, usimamizi wa kodi, pamoja na viwango vya kodi, kwa lengo la kufanya mfumo wa ukusanyaji kuwa rafiki zaidi na kuongeza wigo wa mapato ya Serikali.”
Waziri Mkuu alikuwa akijibu swali la mwezeshaji wa mdahalo huo, Dkt. Joy Kategekwa ambaye pia ni Mkurugenzi wa Uratibu na Ushirikiano wa Kikanda wa Benki ya AfDB ambaye alimtaka Waziri Mkuu aeleze uzoefu wa Tanzania katika usimamizi wa fedha za umma na jinsi ambavyo imefanikiwa kufikia bajeti ya nchi inatumia asimilia 70 ya mapato ya ndani.
Akitoa ufafanuzi zaidi, Dkt. Mwigulu alisema Tanzania iliamua kuimarisha ukusanyaji wa mapato kwa kuiongezea ufanisi Mamlaka ya Mapato ikiwemo kuweka mifumo ya ukusanyaji kwa kutumia njia za kidijitali kama vile mashine za EFD na kufanya malipo kwa njia za mitandao ya simu.
“Mamlaka za Serikali za Mitaa ziliimarishwa kwa kuruhusiwa kukusanya mapato yasiyo ya kikodi na tukahakikisha kuwa kunakuwa na nidhamu ya matumizi ya fedha kwa kila senti inayokusanywa (prudency) na wananchi waliona fedha zao zinatumika katika miradi hiyo,” alisema na kuongeza:
“Tanzania ni miongoni mwa wanufaika wa ushirikiano na Benki ya Maendeleo ya Afrika na tumepata nafasi ya kushirikisha uzoefu wetu kuhusu utekelezaji wa miradi mbalimbali kwa kutumia vyanzo vya ndani vya fedha ikiwemo ujenzi wa Bwawa la Mwalimu Nyerere, miradi ya huduma za jamii, ujenzi wa Chuo Kikuu cha Dodoma, Hospitali ya Benjamin Mkapa pamoja na miradi mingine ya miundombinu iliyotekelezwa kwa kutumia rasilimali za ndani ya nchi.”
Akitoa maelezo ya jumla kuhusu mkutano huo, Waziri Mkuu alisema wakati wa ufunguzi walijadili ajenda kadhaa ikiwemo ripoti za kifedha na mada zilizohusu uhuru wa kiuchumi wa nchi za Afrika na nafasi ya mawakala wa biashara katika maendeleo ya bara la Afrika.
“Katika ufunguzi, tumeelekeza nguvu kubwa katika kujadili namna ambavyo nchi za Afrika zinaweza kuondokana na utegemezi wa vyanzo vya fedha kutoka nje kwa ajili ya utekelezaji wa miradi ya maendeleo na badala yake kujikita zaidi katika matumizi ya vyanzo vya ndani vya mapato na rasilimali zilizopo barani Afrika.”
Alisema sababu kubwa ya mjadala huo ni mabadiliko yanayoendelea duniani ambayo yamesababisha baadhi ya vyanzo vya fedha vilivyozoeleka kama vile misaada na mikopo yenye masharti nafuu kuendelea kupungua kutokana na changamoto mbalimbali za kiuchumi zinazozikabili nchi zilizokuwa zikitoa misaada hiyo.
Waziri Mkuu alisema katika mjadala huo imebainishwa wazi kuwa Afrika bado ina fursa kubwa ya kufanikisha miradi yake ya maendeleo kwa kutumia vyanzo vya ndani. “Miongoni mwa maeneo yaliyotajwa ni matumizi ya mifuko ya hifadhi ya jamii, sekta ya bima, rasilimali za asili, pamoja na utajiri uliopo katika nchi mbalimbali za Afrika. Kwa hiyo, mjadala umeonesha kuwa huu ni wakati sahihi kwa Afrika kuelekeza nguvu zake katika kujitegemea kifedha kupitia matumizi bora ya rasilimali za ndani.”
Hata hivyo, Waziri Mkuu ameeleza, ili kufanikisha hilo ni lazima kuwepo na matumizi bora ya rasilimali hizo, pamoja na kuwekeza katika miradi yenye tija kwa wananchi. Miradi hiyo ni ile inayolenga kuzalisha ajira kwa vijana na wanawake, kukuza uchumi, kuongeza mapato ya ndani na kuhakikisha kunakuwa na uendelevu wa mapato ya Serikali.
Ametaja eneo jingine ambalo limeguswa kuwa ni umuhimu wa teknolojia katika kuchochea maendeleo ya kiuchumi kwani itasaidia kuongeza tija katika uzalishaji, kuboresha ukusanyaji wa mapato na kuongeza ufanisi katika usimamizi wa mifumo mbalimbali ya kiuchumi.
Alisema azimio muhimu ambalo nchi washiriki zimeondoka nalo ni umuhimu wa Serikali za Afrika kuwekeza katika mabadiliko ya kisera, kisheria na kiutawala yatakayowezesha matumizi bora ya fursa zilizopo ikiwemo maboresho ya mifumo ya kodi, usimamizi wa mapato yasiyo ya kodi, usimamizi wa miradi ya maendeleo na kuimarisha mifumo ya utawala wa kifedha.

.jpeg)

.jpeg)

0 Comments