NEWALA: WAKAZI wa Kijiji cha Lidumbe Shuleni katika Halmashauri ya Mji Newala mkoani Mtwara watanufaika na mradi wa ujenzi wa Zahanati ya Kijiji cha Lidumbe yenye thamani ya Sh milioni 105.

Hayo yamejiri wakati Mwenge wa Uhuru mwaka 2026 ulipoweka jiwa la msingi mradi huo wa zahanati hiyo baada ya kupokelewa katika kijiji hicho cha lidumbe ukitokea Halmashauri ya Wilaya ya Tandahimba.

Katika mji huo wa Newala mwenge utapitia miradi 7 ya maendeleo yenye thamani ya ya zaidi ya Sh bilioni 2 ikiwemo ujenzi wa zahanati hiyo ya lidumbe shuleni iliyoanza na nguvu za wananchi, nyumba ya mtumishi zahanati ya kijiji cha msilili.

Pia ujenzi wa kituo cha biashara cha Smon Chikolo, shughuli za kikundi cha business centre, ujenzi wa shule ya sekondari uhuru, ujenzi wa barabara ya nambung-mkoma kilomita 0.8 na mingine.

Akizungumza wakati wa uzinduzi wa zahanati hiyo ya lidumbe shuleni, Mwenyekiti wa Kitongoji cha Dubai kwenye mji huo, Saidi Naunda amesema muda mrefu sasa wamekuwa wakipata huduma ya afya maeneo jirani ikiwemo zahanati ya tawala iliyopo kijiji cha tawala.

“Tunapopata huduma hii kwa ukaribu hapa kijiji kwetu sasa tunafarijika sana sisi wananchi kwasababu tutakuwa tumeondokana na usumbufu wa kwenda mbali kufata huduma”amesema Naunda

Naye mkazi wa kijiji hicho cha lidumbe shuleni, Amina Hassan amesema kupitia mradi huo watanufaika kwenye huduma nyingi za afya ikiwemo huduma ya kliniki kwa watoto, kuondokana na suala la akina mama wajawazito kujifungulia njiani na wengine.

Kiongozi wa Mbio za Mwenge wa Uhuru Kitaifa mwaka 2026, Wazo Mwang’onda amewahakikishia wakazi hao kuwa zahanati hiyo inaenda kukamilika muda siyo mrefu hivyo watapata huduma ya afya.

“Niwapongeze sana wananchi kwa kushirikiana na serikali kuanzisha zahanati hii hivyo niwaombe wananchi mukae mkao wa kula sasa hivi mtapata huduma hapa hapa kijijini kwenu”amesema Wazo