Kwa mujibu wa Naibu Mkuu wa Masuala ya Utamaduni na Jamii wa Manispaa ya Tehran, mazishi ya Ali Khamenei yatafanyika "huenda mwishoni mwa mwezi wa Dhul-Hijjah na mwanzoni mwa mwezi wa Muharram," yaani takribani baada ya wiki mbili.

Mohammad Amin Tavakolizadeh alisema katika mkutano wa 52 wa Tume ya Kijamii na Kitamaduni ya Miji Mikuu ya Iran kwamba jeshi la nchi hiyo ndiyo itakayoratibu shughuli hiyo, na kwamba siku tatu za "maandamano ya wananchi" zimepangwa kama sehemu ya shughuli za mazishi.

Bw. Tavakolizadeh alisema kuwa baada ya hafla ya kuaga mwili, sala za mazishi na taratibu nyingine za maziko zitafanyika, na shughuli hizo zitadumu kwa takribani saa 24 katika mji wa Tehran.

"Tunajiandaa kwa idadi ya watu zaidi ya milioni 15 hadi 20 katika mji mkuu," alisema.

Kwa mujibu wa Tavakolizadeh, baada ya Tehran, shughuli za mazishi zimethibitishwa kufanyika katika miji ya Qom na Mashhad, huku majimbo mbalimbali nchini yakitoa maombi ya kuwa wenyeji wa shughuli hizo za mazishi.

Alisema kuwa mahali pa mazishi ya Ayatollah Ali Khamenei patakuwa katika hekalu ya Imam Reza mjini Mashhad, "kwa kuzingatia wosia wake na mapendekezo ya ndugu zake."

Naibu meya wa Tehran alisema kuwa viongozi na waombolezaji kutoka Pakistan, Afghanistan, India, Bangladesh, Kashmir na maeneo mengine ya ulimwengu wa Kiislamu upande wa mashariki wanatarajiwa kusafiri kwenda Mashhad kuhudhuria shughuli hizo.

Pia alisema kuwa miji iliyoko katika njia ya msafara wa mazishi itakuwa mwenyeji wa hafla za maombolezo kwa angalau siku moja. Miji hiyo ni pamoja na Qom, Karaj, Saveh, Garmsar na Semnan.